CHANZO CHA HOFU NYINGI ULIZONAZO NA ZINAZOKUZUIA USHINDWE KUFANIKIWA
Wapo watu ambao ni waoga sana kuwajibika hasa linapokuja suala la kufanya kile kitu wanachotakiwa kufanya. Utakuta ni watu wa kusingizia sana hiki au kile, kwamba siwezi kufanya kwa sasa, kwa sababu hii au ile.
Kwa mfano, utakuta mtu anataka kuanzisha biashara ya aina fulani, ambapo ukiangalia kama ataanzisha biashara hiyo, itamsaidia sana mtu huyo kuweza kuingiza kipato kikubwa na cha ziada.
Hata hivyo, kitu cha kushangaza au cha ajabu kwa sababu ya hofu ama wasiwasi tu, mtu huyo atajikuta anatoa visingizio vingi sana mpaka kushindwa kuanza biashara hiyo, ambayo ilitakiwa ainze mara moja.
Kitu usichokijua, kisaikolojia unaposhindwa kufanya jambo fulani kwa sababu ya hofu za mara kwa mara, mawazo yako ya ndani, mawazo yanayoumba au kupelekea mambo hutokea, huchukua hofu hiyo na kuihifadhi na kuifanya kama ‘ulemavu’ wako.
Kwa hiyo kila unapojaribu kufanya jambo jipya utakuta wazo linashuka haraka sana ndani yako, ‘Je ukishindwa itakuwaje? Si unaona wengi sana huwa wanashindwa hapo,’? Utashangaa ubongo wako una hofu sana, hata pengine bila kujua kwa nini?.
Lakini ukiangalia, hiyo yote inatokana na hofu ndogo ndogo ambazo ulizibeba sasa zimekaa kwenye mawazo yako ya kina na imekuwa kama ndio ‘ulemavu’ wako wa kiakili yaani 'psychological disorders', sasa kila kitu ukitaka kukifanya unakuwa una hofu.
Kitu cha kujiuliza kwa nini watu wanakuwa na hofu sana hasa pale wanapotaka kuanza jambo fulani? Chanzo hasa huwa nini?
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazopelekea hofu moja kwa moja kwenye maisha yako na kushindwa kuchukua hatua sahihi za majukumu yako.
1. Kuogopa kukosea.
Utakuta hapa hofu inazalishwa sana kwa sababu ya kuogopa kukosea. Utakuta mtu anakuwa ana wasi wasi mwingi hivi jambo hili lisipokwenda sawa itakuwaje? Mwisho wa siku kila kitu hufika mahali kimekwama.
2. Kuogopa kushindwa.
Pia kuna watu ambao wanajawa na hofu kwa sababu ya kuogopa kushindwa. Kwa watu kama hawa kwao wanaona inakuwa ni bora wasifanye kabisa kuliko wakafanya halafu wakashindwa. Kwa lugha rahisi watu wenye hofu hii huwa hawafanikiwi.
.3. Kutokujiamini.
Unaposhindwa kujiamini, elewa kabisa huwezi kufanikiwa katika kitu chochote. Kujiamani mara nyingi ndio msingi wa mafanikio. Waangalie watu ambao wanajiamini utakuta ni watu ambao wanamafanikio wakati wasiojiamini hawana kitu maishani mwao.
4. Kuogopa ushindani.
Mwingine utakuta anashindwa kuanza jambo analotakiwa afanye, inaweza kuwa biashara au kitu chochote eti kisa kwa sababu ya kuogopa ushindani. Kwa jinsi anavyoogopa ushindani anajikuta hawezi tena kufanya kitu.
5. Kukosa hamasa.
Pia ni rahisi sana kuanza kuingiwa na hofu kama umekosa hamasa ya kile unachokifanya. Ni muhimu sana kuwa na hamasa ili ikusaidie kukujaza ujasiri wa kufanya hicho unachokifaya kwenye maisha yako.
6. Mawazo hasi.
Kama una mawazo sana kama vile ‘aah mimi sina uwezo wa kufanikisha hili, huu mradi sio saizi yangu,’ uwe na uhakika hutaweza kufanya kwa ujasiri, hapo utakuwa unajijaza hofu mwenyewe zitakazo kufanya ushindwe tu.
Kimsingi, kuogopa kushindwa, kuogopa ushindani, kugopa kukosea, kukosa hamasa, mawazo hasi na kutokujiamini ni moja ya sababu zinazokufanya wewe uwe na hofu kubwa kwenye maisha yako
No comments
Post a Comment