Magavana na wabunge wa Kenya waliopoteza viti vyao mahakamani
Majaji wa mahakama ya juu nchini Kenya |
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Agosti 8, 2017 na kufuatiwa na uamuzi wa mahakama ya juu nchini humo wa kufutiliwa mbali ushindi wa Uhuru Kenyatta, baadhi ya walioshindwa walipata matumaini na kuwasilisha kesi dhidi ya wapinzani wao.
Leo ilikuwa siku ya mwisho kwa mahakama kutoa uamuzi kuhusu kesi zilizowasilishwa kuhusu uchaguzi huo na kufikia sasa magavana watatu wamepoteza viti vyao na wabunge wanane.
Magavana
Martin Wambora
Katika orodha ya magavana waliopoteza viti vyao baada ya wapinzani wao kupeleka kesi katika Mahakama Kuu; wa kwanza alikuwa Bwana Martin Wambora, Gavana wa kaunti ya Embu. Na miongoni mwa makosa yaliyotajwa yalifanyika, ni ukosefu wa uwazi katika zoezi hilo. Jaji alisema kuwa fomu nambari 37A katika vituo 12 vya upigaji kura zilikosekana, huku karatasi za kupigia kura zikikosa alama maalum iliyohitajika.
Mohamed Abdi
Uchaguzi wa kiti cha Ugavana katika kaunti ya Wajir, pia umefutiliwa mbali, huku Jaji wa Mahakama ya juu Alfred Mabeya, akisema kuwa shughuli hizo hazikufuata sheria.
Pia ilibainika kuwa stakhabadhi za masomo ya Gavana Mohamed Abdihazikuwa zote, na pia ana shahada feki ya Chuo Kikuu.
Maafisa wa IEBC wakihesabu kura nchini Kenya |
Cyprian Awiti
Februari 20, Gavana wa Homa Bay Cyprian Awiti, alishtuliwa mno na uamuzi wa mahakama ya juu, baada ya uteuzi wake kama gavana wa kaunti hiyo, kutupailiwa mbali.
Jaji Joseph Karanja, alisema katika uamuzi huo kuwa tume ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC) haikuendesha uchaguzi wa huru na haki. Alitangaza marudio ya uchaguzi mwingine ufanyike katika kipindi cha siku 60 zijazo.
Mawakili waliokuwa wakishiriki kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8 |
Wabunge
Babu Owino
Na mapema siku ya Ijumaa, mbunge wa Embakasi Mashariki, Bwana Babu Owino, amekuwa mbunge wa 6 kupoteza kiti chake, baada ya mpinzani wake Francis Mureithi, kuwasilisha kesi mahakamani.
Mahakama Kuu imesema kuwa uchaguzi wa Agosti 8, 2017, ambao Bwana Owino alitangazwa mshindi, ulikumbwa na makosa mengi na uvunjaji wa sheria.
Jaji katika kesi ya Bwana Babu Owino, ambaye zamani alikuwa kinara mkuu wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, na ambaye amezuiwa korokoroni mara kadha kwa kutuhumiwa kumtukana Rais Uhuru Kenyatta, ilisikizwa na kuamuliwa na Jaji Joseph Sergon.
Chris Karan
Mbunge wa Ugenya Chris Odhiambo Karan, ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamepoteza viti vyao baada ya mpinzani wake David Ochieng kupinga kuchaguliwa kwake katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mahakama Kuu mjini Kisumu,chini ya Jaji Tripsisa Cherere, iliamua kesi hiyo na kusema kuwa, kampeini ya Bwana Karan ilikuwa ya "kupotosha na utovu wa maadili" na kwamba zoezi nzima ya uchaguzi mkuu huko Ugenya, ulikumbwa na udanyanyifu mwingi. Pigo lingine alilopata Bwana Karan ni kulipa Dola 70,000 kama malipo ya gharama ya kesi hiyo.
Wanjiku Kibe
Mwezi Mpya huu wa Machi 1, Mahakama Kuu mjini Kiambu, ilitupilia mbali ushindi wa Bi Wanjiku Kibe kama mbunge wa Gatundu Kaskazini.
Mahakama hiyo ilisema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu mkubwa hasa ndani tume ya kusimamia uchaguzi nchini Kenya- IEBC.
Mlalamishi katika kesi hiyo, alikuwa mbunge wa zamani Clement Waibara.
Alfred Keter
Mbunge mbishani wa chama tawala cha Jubilee, ambaye anawakilisha eneo bunge la Nandi Hills katika maeneo anakotoka naibu Rais William Ruto la Bonde la Ufa, Bwana Alfred Keter, alipoteza kiti chake Alhamisi ya wiki iliyopita, baada ya Jaji wa mahakama kuu mjini Eldoret, Kanyi Kimondo, alipoamua kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro chungu nzima. Mara baada ya uamuzi huo wa mahakama, Bwana Keter aliwahutubia wafuasi wake na akamkashifu moja kwa moja naibu Rais kwa masaibu haya yote anayopitia.
Kangogo Bowen
Mwenzake wa eneo bunge la Marakwet Mashariki, Bwana Kangogo Bowen ambao wote mara kwa mara wamekuwa wakimkashifu Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, baada ya kuondolewa katika kamati maalum za bunge, pia alikabiliwa na kisu hicho hicho cha mahakama kuu.
Uchaguzi huo sasa utarudiwa, kwani jaji huyo huyo George Kimondo, ndiye aliyeamua ya Bwan Bowen.
Mahakama hiyo ilisema kuwa, vituo viwili vya kupigia kura, havikuwa vimeorodheshwa kwenye gazeti rasmi la serikali lakini vilitumika kusawazishia matokeo ya kura kabla ya kutumwa Nairobi.
Mtambo wa kuwatambua wapiga kura |
No comments
Post a Comment