MWAKYEMBE AWAHAKIKISHIA WANANCHI KUWA SERIKALI HAINA UGOMVI NA WASANII
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewahakikishia wananchi kuwa serikali haina ugomvi wowote na wasanii nchini bali wanachofanya ni kusimamia maadili katika kazi zao wanazozifanya.
Dkt. Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo (Machi 28, 2018) baada ya kupita siku kadhaa tokea Naibu Waziri wa wizara yake Juliana Shonza kutoa tamko la kuzifungia baadhi ya kazi za wasanii zilizokosa maadili katika jamii na kupelekea kuleta utata mkubwa kutoka na wengi wao kutokujua dhamira ya serikali ni ipi.
"Maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo yanafanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa kiongozi wa Wizara, hivyo basi ieleweke kwamba hatua zilizochukuliwa na Naibu Waziri Shonza hivi karibuni zilikuwa za Wizara kwa mujibu wa sheria za nchi", amesema Dkt. Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Dkt. Mwakyembe ameendelea kwa kusema "serikali haina ugomvi wowote na wasanii nchini bali jukumu ni kusimamia maadili hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema enzi za uhai wake kwamba taifa lisilo na utamaduni wake ni sawa na taifa mfu, hivyi nawaagiza watendaji wa Wizara na Taasisi zake ikiwemo BASATA, Bodi ya filamu Tanzania na TCRA mkutane na makundi ya wasanii wa muziki muwape elimu kuhusu taratibu za kuwasha kazi zao mamlaka husika ili kujiridhisha na maudhui ya kazi hizo kabla ya kuzisambaza".
Kwa upande wake Naibu Waziri Shonza amewasisitizia wasanii umuhimu wa kufuata utaratibu kwa kuwasilisha kazi zao kwenye mamlaka husika ili kuepusha matatizo ambayo yanayoweza kutokea hapo baadae.
No comments
Post a Comment