. . Mzee aliyegundua Tanzanite ataka kuonana na Rais Magufuli
Mzee Ngoma (79) amesema amekuja Dar es salaam kupata fursa hiyo ya kuonana naye ili amsaidie kwani licha ya kuwa na jina kubwa na kufanya mambo makubwa katika nchi hii lakini bado serikali haioni umuhimu wake kwani amekuwa akifuatilia kupata japo stahiki yake.
Akieleza sababu kubwa inayompelekea kumuona Rais Magufuli, Mzee Ngoma amesema wanakijiji huko anakotoka hawaamini na wanamcheka kwani hali yake ni ngumu kimaisha na afya yake imekuwa ikidhoofu kwa magonjwa bila hata kupata matibabu kutoka serikalini.
Mzee Ngoma amesema wazo la kufikia hatua ya kuongea kwenye vyombo vya habari kutaka aonane na Rais Magufuli, limekuja baada ya juhudi za kuhangaika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, RC Makonda kugonga mwamba, ambapo alitaka amfikishie ombi hilo ili ampelekee Rais Magufuli. Tazama video ya mzee hiyo akiongea juu ya dhumuni lake la kuonana na Rais Magufuli.
Jumanne Mhero Ngoma amezaliwa mwaka 1939 na ndiye Mtanzania aliyegundua madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania pekee. Uguduzi huu ulifanyika tarehe kama ya leo, 23 Septemba 1967. Madini haya yanapatika eneo la Mererani mkoani Arusha.
Mzee Ngoma alipewa tuzo kwa ugunduzi wa madini ya Tanzanite mwaka 1984. wakati akipokea cheti hicho alieleza kuwa “Mara ya kwanza kuyagundua madini haya nilikuwa mdogo sana. Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa porini nikichunga mifugo. Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai walikuwa wameupa jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa linafahamika kwa jina la Naisunyai ambako kwa kawaida Wamasai walikuwa wakilitumia kunywesha mifugo yao,“.
Anaendelea kueleza Mzee Ngoma “Siku hiyo niliona vitu vinavyowakawaka. Nikawa najiuliza vitakuwa ni vitu gani? Awali nilidhani pengine ni nyoka au wanyama wa hatari. Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari kwa lolote. Nilipogusa na mti niliokuwa nimeushika, nikashangaa mawe yanayong’aa yakitoka ardhini. Vipande vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu. Kwa kweli nilivipenda sana.”
Mzee ngoma kwa sasa anasumbuliwa na matatizo ya kupooza ambapo watoto wake wameitaka serikali imchukulie kwa ukubwa kama watu wengine mashuhuri wanavyopewa matibabu.
No comments
Post a Comment