Followers

Nape Nnauye aipa ushauri Serikali




Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Nape Nnauye ameishauli Serikali kuboresha mipaka ya nchi kwa wakati ili kuondokana na migogoro inayojitokeza mara kwa mara kufuatia uvamizi wa wahamiaji kutoka nchi jirani.


Ameyasema hayo katika ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembea mipaka kati ya Tanzania na Uganda Wilaya ya Missenyi upande wa Tanzania Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Isingiro upande wa Uganda.

Nape amesema suala la kulinda mipaka ni muhimu hivyo ni vyema serikali kupitia Wizara ya Ardhi ikatenga fedha za kutengeneza barabara zilizoko mipakani ili kurahisisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu na kuwezesha wakazi wa nchi hizi mbili kutambua mipaka ili kuepusha migogoro ya matumizi ya ardhi.
“Tumebaini kuwa kuingia kwa wananchi wa Uganda hasa kuleta mifugo yao katika lanchi ya Missenyi kunachangiwa na kutokuwepo njia maalumu na alama maalumu zinazotenganisha kati ya nchi na nchi hivyo watu wanaingia kupitia katika vichochoro visivyo rasmi na kuhatarisha amani kwa wakazi wa mipakani alisema Nnauye”
Kamati hiyo pia ilifanikiwa kufika katika vijiji vya Rwengiri, Bwenkoma na Bubale vilivyopo kata ya Kakunyu na kubaini kuwa baadhi ya alama zilizowekwa mpakani zimepotea hivyo wafugaji kutoka maeneo mbalimbali wanaendelea na shughuli za ufugaji bila kujali sheria.

Mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Denice Mwila amesema kuwa kamati ya ulinzi na usalama imekuwa ikikagua mipaka na kutatua changamoto mbalimbali hivyo kama barabara itatengenezwa katika mipaka yote ya Missenyi kazi ya kuwabaini waarifu itakuwa rahisi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula amesema kuwa mpaka sasa Wizara imepokea shilingi bilioni 4 za kuimarisha mipaka ambapo fedha zitakazotumika kuimarisha mpaka wa Tanzania na Uganda ni shilingi Bilioni 1.9 na shilingi Bilioni 2.1 kwa mpaka wa Tanzania na Kenya.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.