Wastara Arejea, Asema Fedha za Matibabu Hazikutosha
Msanii wa filamu, Wastara Juma amerejea nchini leo akitokea Mumbay nchini India alikokuwa anapatiwa matibabu ya mgongo na mguu na kuwashukuru Watanzania kwa namna walivyojitokeza kumchangia fedha za matibabu, ingawa hazikutosha na kulazimika kuuza baadhi ya mali zake.
Akizungumza na MCL Digital leo Machi 1, 2018 nyumbani kwake Tabata ikiwa ni saa chache baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, amesema baada ya kufika hospitali alikutwa na matatizo mengine zaidi ya aliyokuwa nayo jambo lililosababisha gharama za matibabu kuwa kubwa.
Wastara alifanikiwa kwenda kwenye matibabu hayo, Februari 3, 2018 baada ya kupata michango kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli aliyemchangia Sh15 milioni.
Amebainisha kuwa matatizo aliyokutwa nayo ni pamoja na uvimbe chini ya kalio na kwamba, ndilo lilikuwa sababu ya kukaukiwa damu pamoja na kubainika kuwa na uvimbe kichwani uliotokana na kupata ajali zaidi ya mara tatu.
“Kutokana na matatizo haya ilifika mahali pesa nilizokwenda nazo ziliniishia na kulazimika kuwaomba ndugu zangu wauze baadhi ya mali zangu, ikiwemo kamera ili niweze kuendelea na matibabu,” amesema.
“Mtu umeshafika kwenye matibabu tena nchi za watu unafanyaje? Kurudi bila kutibiwa huwezi. Nililazimika kuwasiliana na ndugu zangu ili wauze baadhi ya vitu vyangu niweze kutibiwa maana afya yangu ni muhimu kuliko kamera.”
No comments
Post a Comment