Followers

ANGALIA BABU MBARONI KWA KUOA KATOTO MIAKA 12,DUNIA INAKOELEKEA NI MAJANGA

AMA kweli dunia imekwisha! Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ na Serikali ya Awamu ya Tano wakipinga vikali kukatisha ndoto za watoto kusoma kwa kuwapa mimba au kuwafungisha ndoa wakiwa na umri mdogo, babu wa mwenye umri wa miaka 70, Mzee John Mkubila anadaiwa kumchezea rais sharubu, Ijumaa Wikienda limedokezwa.

Mzee Mkubila ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa kosa la ‘kukaoa katoto ka’ miaka 12’ ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba (jina la binti linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili). Tukio hilo lilijiri hivi karibuni katika Kitongoji cha Rwenge Kijiji cha Bugalama mkoani Geita ambako ndiko familia hizo zinapoishi.

TUJIUNGE NA CHANZO Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho ni shuhuda wetu, mzee huyo ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mwembeni Kata ya Nyankumbu mjini Geita alikiri mbele ya polisi kumuoa binti huyo kwa makubaliano na mzazi wa binti huyo. Alisema kuwa, babu huyo aliomba kumuoa mtoto huyo ili awe anamsaidia kazi za nyumbani kwa kuwa mkewe ana majukumu mengi ya kibiashara. “Mzee alisema kutokana na mkewe kuwa bize alijikuta huduma za msingi na kuamua kumuoa binti huyo,” alisema shuhuda huyo.

MSIKIE MZEE MWENYEWE Kwa upande wake mzee huyo alilieleza Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita: “Nilionana na baba yake, nikamwambia kuwa kwa sasa umri wangu umekwenda, je, ninaweza kupata binti mdogo wa kunisaidia maana kwangu nina mke ila ana majukumu mengi hivyo ninajikuta nashindwa kufanya shughuli nyingine. “Baba yake aliniambia sawa, ndiyo akawa amenipa huyu binti ambaye kwa sasa ni mke mdogo.”

HUYU HAPA BINTI Kwa upande wake mtoto huyo alikiri kuolewa na mzee huyo kutokana na baba yake mzazi kumlazimisha. “Mimi nilikataa kuolewa, baba yangu ndiye ambaye alinilazimisha niolewe ila mimi sikuwa tayari kuolewa kutokana na umri wangu kuwa mdogo,” alisema binti huyo mbele ya polisi.

ISHU IMEKAA VIBAYA Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye ofisi za polisi jamii kwenye mtaa huo ambao ndiyo waliobumburua ishu hiyo walionesha kusikitishwa na tukio hilo huku wakikiri kwamba huko ni kumchezea sharubu JPM ambaye ameshakataza mambo hayo. “Huku ni kumchokoza Rais JPM maana alishasema hajaribiwi. Kiukweli jamii inapaswa kubadilika na kuachana na desturi ambazo zimeendelea kuwakandamiza watoto wa kike hivyo hii ishu imemkalia vibaya huyu mzee,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Innocent.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Mponjoli Mwabulambo alisema kuwa nyuma ya tukio hilo kulikuwa na mapatano baina ya wazazi wa mtoto na mzee huyo kama mahari ilitolewa, lakini pia uchunguzi unafanyika na utakapokamilika wote watafikishwa mahakamani kwa kuwa ni kosa la kisheria kujamiana na mtoto mwenye umri wa chini ya miaka kumi na tano (15). Stori: Mwandishi Wetu,

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.