Jpm Afunga Mjadala Wa Trilion 1.5 Tzsh Ripoti Ya [CAG
Rais Magufuli Amewashangaa Wanao eneza uvumi wa upotevu wa kiasi hicho cha Fedha na kusema jana ikulu kwamba Hakuna kitu Kama hicho ni Uvumi Usio Na Maana
Rais Dk. John Pombe Magufuli akiwapongeza Majaji, baada ya kuwaapisha, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU
Taarifa kuhusu upotevu wa fedha hizo ilidaiwa kuwapo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huku akisisitiza kuwa kama zingepotea angeshafukuza mawaziri na maofisa wengine waliohusika siku hiyo hiyo ya kupokea ripoti.
Aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha majaji wapya 10, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.
Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwake na taarifa ambazo zimezagaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kwenye ripoti hiyo kuna kiasi hicho cha fedha ambazo zimepotea ingawa ni uongo mtupu.
Hoja ya kupotea kwa fedha hizo kwenye ripoti ya ukaguzi ya (CAG), iliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, na imekuwa mjadala mkubwa bungeni na kwenye mitandao ya kijamii.
“Kama nilifukuza wakurugenzi watatu wa halmashauri siku hiyo hiyo nilipopokea ripoti ya CAG, ningeshindwaje kufukuza waliotafuna hizo fedha? Hata angekuwa waziri ningeshamfukuza siku hiyo,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuna ugonjwa ambao umeingia Tanzania wa watu kudhani kwamba kila kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni cha kweli na kwamba hayo yote yamesababishwa na uhuru wa watu kutuma vitu kwenye mitandao hiyo bila kudhibitiwa.
Alisema kwa kuwa Tanzania haina uwezo wa kuidhibiti mitandao hiyo wako watu wa nje ya nchi ambao wamekuwa wakiitumia kwa maslahi yao bila kujali madhara ambayo yanaweza kutokea.
“Nilishangaa sana kusikia wanasema serikali imepoteza (Sh.) trilioni 1.5. Niliisoma ripoti ya CAG mara mbili mbili sikuona hiyo sehemu, nikampigia CAG kumwuliza mbona kwenye ripoti yako hukunisomea wizi huo? CAG aliniambia hakuna kitu kama hicho, nikajaribu kusoma ripoti nzima sikuona hizo trilioni 1.5 zilizopotea, Nikampigia Katibu Mkuu Hazina naye akaniambia hakuna kitu kama hicho,” alisema Rais Magufuli.
Kwenye hafla hiyo ya jana ambayo ilirushwa moja kwa moja na baadhi ya vyombo vya habari, Rais Magufuli alimwinua CAG, Profesa Mussa Assad, ili aueleze umma wa Watanzania kama kuna kiasi hicho cha fedha kilichoibwa lakini alikanusha kwamba habari hizo si za kweli.
“Kwa bahati nzuri CAG upo hapa hebu simama useme kama tuliibiwa trilioni 1.5, (CAG alijibu kwamba hakuna kitu kama hicho) au Katibu Mkuu Hazina na wewe sema kama tuliibiwa trilioni 1.5,” Katibu Mkuu Hazina alisimama na kusema “Sisi Hazina tuko vizuri.”
Aidha, Rais Magufuli alisema uhuru wa watu kutuma vitu kwenye mitandao ya kijamii bila kudhibitiwa ndiyo umesababisha yote hayo na kwamba watu wanaofanya hivyo wamekuwa wakijenga hoja na kuwaaminisha Watanzania kuwa wanachosema ni cha kweli.
“Yaani mtu anakaa anaandika wala hamwogopi Mungu, anatuma chochote na kuwaaminisha watu kwamba kuna hela zimeibwa. Zingeibwa ningefukuza hata waziri siku hiyo hiyo maana hatuwezi kuwa tunatafuta hela halafu zinaibwa na hata nilipomuuliza CAG hawa watu umewaficha wapi akasema hakuna,” alisema Rais Magufuli.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu wewe ni jaji na hayo yanayokupata huko na sisi huku serikalini yanatukuta sana, naona ni wakati muafaka tuanze kuzitumia sheria zetu maana ukishapotosha watu madhara ni makubwa sana. Tunaweza kuchukulia kawaida lakini madhara yake ni makubwa, Mtu anapotosha watu milioni 55 na wengine wameanza kuamini,” alisema
“Fikiria aliyeandika hii ripoti yupo na ni profesa lakini watu wanapotosha makusudi, sasa DPP yupo, Wakili Mkuu wa Serikali yupo, manaibu na nyinyi mpo, majaji mpo najua zikija kesi kama hizi mtazishughulikia haraka haraka, lazima tuweke uzalendo mbele maana nchi hii ikiharibika hakuna mtu atakayebaki salama, madhara ni makubwa mno,” alisema
KAULI YA WIZARA
Kutoka Bungeni mkoani Dodoma, serikali imetolea ufafanuzi ziliko Sh. trilioni 1.51, ambazo ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2016/17 ulibaini matumizi yake hayaonekani.
Imesema Sh. bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh. bilioni 689.3 ni mapato tarajiwa na Sh. bilioni 203.9 ni mapato ya yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo bungeni mjini hapa jana alipotoa kauli ya serikali kuhusu suala hilo.
Alisema katika uandishi wa taarifa ya CAG, kulitumika taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti na kwamba hadi Juni 2017, mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh. trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa Sh. trilioni 23.79.
“Matumizi haya hayakujumuisha Sh. bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za serikali zilizoiva," Dk. Kijaji alisema kueleza zaidi:
"Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika, hivyo basi baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh. trilioni 24.4."
Naibu waziri huyo alisema katika kipindi cha mwaka wa 2012/2013 hadi mwaka 2016/2017, serikali ilikuwa katika kipindi cha mpito cha kutekeleza mpango mkakati wa kuandaa mapato ya serikali kwa kutumia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma, yaani International Public Sector Accounting Standards (IPSAS Accrual)
Alisema kuwa katika kipindi hicho, serikali ilitumia mfumo huo kukusanya hesabu za mapato na matumizi ya serikali kuiwezesha kikamilifu kutambua hesabu za mali, madeni na makusanyo ya kodi.
Alisema IPSAS Accrual ni mfumo ambao mapato na matumizi yanatambuliwa baada ya muamala husika kukamilika na si hadi pesa taslimu inapopokewa ama kutolewa.
Alisema matokeo ya utekelezaji wa mfumo huo yameiwezesha serikali kutoa taarifa za uwazi katika taasisi zake na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mipango.
Alisema hakuna fedha ya kiasi cha Sh. trilioni 1.5 zilizopotea au kutumika bika kuidhinishwa na Bunge, bali ni kutokana na serikali kutumia mfumo wa IPSAS Accrual.
"Napenda kulitaarifu Bunge na wananchi kwa ujumla kuwa, serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Pombe Magufuli, ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za umma," Dk. Kijaji alisema na kuongeza:
"Dhamira ya serikali ni kuona kila mapato yanayokusanywa yanatumika ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania." Kauli hiyo ya serikali ilitolewa baada ya Bunge kukatisha kipindi cha 'Maswali', jambo lililofanya baadhi ya wabunge kuhoji sababu za kanuni kuvunjwa.
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema), aliomba mwongozo akisema kanuni zinataka kipindi cha 'Maswali' kiwe dakika 60, hivyo kutaka Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa anaongoza kikao, ampe sababu za kukatisha kipindi hicho kinyume cha kanuni.
Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema hakuna kanuni iliyovunjwa kwa sababu maswali mawili ambayo yalibaki jana bila kujibiwa, yatapangiwa utaratibu mwingine.
No comments
Post a Comment