Kenya yaanzisha mpango wa barabara za ‘mwendo kasi’
Serikali ya Kenya imeanza mpango wa kutenga mkondo mmoja kwenye barabara kuu ya Thika wa kutumiwa na mabasi ya kubeba abiria jijini Nairobi.
Waziri wa uchukuzi nchini humo James Macharia amesema mpango huo ambao utaanza kutekelezwa mara moja unalenga kupunguza msongamano wa magari jijini Nairobi.
Bw Macharia akizungumza katika mkutano wa kamati ya Bunge la Seneti kuhusu barabara nchini humo amesema mpango huo umeanza kutekelezwa.
Barabara ya Thika ni miongoni mwa barabara sita kuu za kuingia na kutoka jijini Nairobi ambazo zinaangaziwa na serikali kwa sasa katika juhudi za kupunguza msongamano.
Bw Macharia amesema mpango huo pia utachangia kushuka kwa nauli.
"Tunahitaji zaidi ya mabasi 900 katika njia hizi sita kuu za kuingia na kutoka jijini lakini kwa sababu hatuna mabasi hayo, tumefungua njia moja, barabara kuu ya Thika," amesema Bw Macharia kwa mujibu wa gazeti la Nation.
Huku waziri huyo akitoa tangazo hilo, shughuli ya kuchora na kuweka alama katika mkondo wa barabara hiyo wa kutumiwa na mabasi ya uchukuzi wa umma tayari imeanza.
- Rwanda kudhibiti mwendo kasi
- India kujenga treni ya kwanza ya mwendo kasi
- Tanzania yaanza kujenga reli ya kisasa
Baadhi ya Wakenya mtandaoni hata hivyo hawajaunga mkono mpango huo, kama walivyoandika wawili hawa kwenye Twitter.
Bw Macharia awali alikuwa amesema serikali ilikuwa inaangazia utekelezwaji wa mifumo miwili mikuu ya kupunguza msongamano wa magari katika miji, moja wa mabasi ya mwendo kasi maarufu kama Bus Rapid Transport System (BRTS) na mwingine wa kusafirisha watu wengi kwa pamoja ambao hushirikisha pia treni, maarufu kama Mass Rapid Transit System (MRTS)
"Kwa sababu za kimipango na kifedha, tumeanza kuuteketeleza mpango wa BRTS kwa kuupa kipaumbele na kwa dharura," aliambia gazeti la Star.
"Kuanzia wiki ijayo, tutakuwa na mkondo maalum wa mabasi haya ambapo tutaanza na ambasi yanayosimamiwa na wahudumu wa Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS)."
NYS ilianza kusafirisha abiria siku chache zilitopita katika barabara zianzoelekea mitaa yenye watu wengi Nairobi, hatua iliyopingwa vikali na wahudumu wa kibinafsi katika sekta ya uchukuzi wa umma.
Kwa mujibu wa Bw Macharia, serikali itakuwa na jumla ya mabasi 100 na sekta ya kibinafsi inatarajiwa pia kuwa na mabasi mengine kama hayo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Aidha, ni mabasi yenye kuwabeba watu wengi kwa pamoja pekee ambayo yataruhusiwa kuingia ndani ya mji.
"Tunawasiliana na Hazina Kuu kuhusu mpango wa kuweka nafuu kwenye kodi ya uagizaji wa mabasi haya ili kuharakisha uingizwaji wake nchini," amesema.
Wahudumu wa kibinafsi wakiongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) Simon Kimutai na Waziri wa Utumishi wa Umma Dkt Margaret Kobia walitofautiana mbele ya kamati ya bunge kuhusu mpango huo Jumatano.
Bw Kimutai anasema serikali haifai kuingilia shughuli ya uchukuzi wa abiria ambayo imekuwa ikifanywa na sekta ya kibinafsi.
Lakini Dkt Kobia alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuna huduma bora ya uchukuzi kwa raia wake.
Mkuu wa polisi Kenya Joseph Boinnet Jumatano alisema barabara ambazo zitashirikishwa katika mpango huo wa kuwa na mkondo maalum tayari zimetengwa.
"Hii ni shughulia mabyo tunaunga mkono kikamilifu na tulikuwa pia tunaunga mkono mpango uliozinduliwa na NYS wa Operation Okoa Abiria," alisema.
Kwa mujibu wa Bw Boinner, mikondo hiyo maalum kwenye barabara itatumiwa na mabasi ya NYS na mabasi ya watu binafsi.
Mpango wa kuwa na maeneo maalum ya kutumiwa na mabasi maalum ulianza kujadiliwa mara ya kwanza mwaka 2008 lakini hatua za kuutekeleza zilikuwa bado hazijachukuliwa.
Mpango huo wa kutenga maeneo maalum kwenye barabara umeanza kutekelezwa huku taarifa zikieleza kuwa serikali ya baraza la jiji imetoa makataa ya siku 10 kwa magari ya uchukuzi wa umma yanayomilikiwa na watu binafsi kutoingia tena katikati mwa jiji.
Waziri wa uchukuzi katika serikali ya baraza la jiji Mohamed Dagane aliambia gazeti la Star kwamba mabasi ya watu binafsi yatakuwa yakiwafikisha abiria hadi vituo vya mabasi vilivyo pembeni mwa jiji.
Mabasi ya NYS ndiyo yatakayokuwa yakiwaingiza abiria katikati mwa jiji kwa mujibu wa Bw Dagane, ambapo mabasi 27 yatatumiwa katika shughuli hiyo.
Ilani ya kuzuia mabasi ya watu binafsi kuingia katikati mwa jiji ilichapishwa Mei 24 mwaka uliopita na ilifaa kuanza kutekelezwa Agosti lakini Gavana Mike Sonko akaahirisha utekelezaji wake.
Mafanikio ya Tanzania
Tanzania ni moja ya mataifa machache ambayo yamefanikiwa kutekeleza mpango wa BRTS ambapo barabara maalum ya kutumiwa na mabasi ya mwendo kasi zilijengwa kwa ushirikiano kati ya taifa hilo na Benki ya Dunia.
Chini ya awamu ya kwanza, mabasi hayo yalipunguza muda wa kusafiri kwa dakika 90 kwa kila abiria kila siku.
Mabasi hayo yamekuwa yakisafirisha abiria, 28,000 kwa saa, ambayo ni jumla ya abiria 400,000 kwa siku.
Mradi huo ulitekelezwa kwenye barabara ya umbali wa kilomita 29.9 ambapo mabasi husafiri kwa mwendo wa wastani wa kilomita 50 kwa saa.
No comments
Post a Comment