Maandamano dhidi ya utawala wa Magufuli yafanyika Washington
Tanzania inajaribu kuzuia maandamano makubwa yaliyopangwa kufanyika Alhamisi, ambayo yameitishwa kupitia mitandao ya jamii kupinga kitendo cha kuzuia uhuru wa kuendesha siasa na uhuru wa vyombo vya habari.
Akaunti ya Mambe Kimambi ya Instagram ikionyesha ujumbe huu.
Rais John Magufuli tangia achukue madaraka miaka mitatu iliyopita inadaiwa kuwa ameendelea kuingilia kati uhuru huo wa wanasiasa na vyombo vya habari.
Maafisa wa polisi wamewaonya wananchi kutokushiriki katika maadamano mitaani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, moja ya nchi za Afrika ambazo zina amani zaidi. Maandamano pia yameandaliwa kufanyika kuelekea katika balozi za Tanzania nchi za nje, ikiwemo ubalozi wa Tanzania mjini Washington, ambapo takriban dazeni za watu waliandamana mapema Jumatano asubuhi.
Baadhi ya watu hao walikuwa wameficha nyuso zao wakati wakiuzunguka ubalozi huo huku kukiwa na mvua ya rasharasha, wakiwa wamebeba mabango yaliokuwa yameandikwa “Mangufool must go!”
“Kila mtu anamuogopa rais na utawala wake,” amesema Mange Kimambi, mwanaharakati wa kisiasa anayeishi California ambaye amekuwa akihamasisha maandamano kutoka katika akaunti yake ya mtandao wa Instagram. “Kwa hiyo nimekuja hapa kuonyesha mshikamano wangu na kuwaunga mkono wao waendelee kusimamia haki zao na kufanya juhudi ya kumuondoa katika madaraka.”
Balozi wa Tanzania Marekani, Wilson Masilingi, hakuweza kupatikana kutoa maelezo yake kwa VOA.
Maandamano yenyewe hasa yamepangwa kufanyika Alhamisi, siku ya kuadhimisha Sikukuu ya Muungano wa Tanzania. Sikukuu hiyo inaadhimisha kuungana kwa nchi mbili Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Siku ya Jumanne, polisi tayari walikuwa wanafanya mazoezi katika mitaa ya mjini Moshi, ambako ni ngome kubwa ya chama cha upinzani Chadema, vyombo vya habari vimeripoti.
Mjini Dar es Salaam, makao mkuu ya zamani ya Tanzania, Mkuu wa Polisi Sweethbert Njewele amesema vyombo vya usalama vilikuwa vinajiandaa kuingia mitaani. Lakini kwa mujibu wa gazeti la The Citizen, tovuti ya habari, alikuwa amewahakikishia kikundi cha wafanyabiashara Jumatano kuwa “hakutakuwa na maandamano. Kila mtu aendelee na shughuli zake kama kawaida.”
Ubalozi wa Marekani umetoa ilani Jumanne, ukishauri kuwa maafisa wa serikali ya Tanzania walikuwa wameonya kuwa kutakuwa na “madhara makubwa” kwa waandamanaji na siku za nyuma polisi walikuwa wametumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuvunja maandamano.
Onyo hilo pia limesema kuwa “ Serikali ya Marekani imezuia Peace Corps wanaojitolea nchini kote kutotoka nje [Alhamisi]” lakini hakuna Mmarekani yoyote mwengine aliyeko nchini kikazi ametakiwa kujizuia nyumbani kwake.
Magufuli tangu achukue madaraka mwaka 2015, ameanzisha mabadiliko magumu ya kiuchumi na kuwakamata wanaojihusisha na rushwa. Pia amezifuta leseni na shughuli za vyombo vya habari ambazo zimekuwa zikionekana kuwa zinakosoa utawala wake.
Ijumaa iliyopita, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imetoa amri kwa wanaendesha mitando ya jamii kuomba leseni kwa kulipa dola za Marekani 900 au watakabiliwa na faini na kifungo cha hadi mwaka moja. Wamiliki hao wamepewa muda hadi Mei 5 kuwa wamesajiliwa.
Mmoja wa wakosoaji wakuu wa Magufuli ni Kimambi, ambaye anaishi Los Angeles. Mama huyo mwenye umri wa miaka 38 na watoto watatu anatumia akaunti yake ya Instagram kukosoa serikali ya Tanzania, rais wake na maafisa wa serikali, na kuwahamasisha wafuasi wake milioni 1.8 kuandamana Alhamisi nchini Tanzania na pia katika balozi za nchi hiyo duniani kote.
Magufuli ameonya kuwa vyombo vya usalama vitawashughulikia wote watakao shiriki katika maandamano hayo ambayo ni “kinyume cha sheria”.
“Baadhi ya watu wameshindwa kushiriki katika siasa kwa kufuata sheria; wanapenda kuona maandamano kila siku mitaani. …Waache waandamane na watanitambua kuwa mimi ni nani,” Rais amesema katika mkutano wa hadhara mapema mwezi Machi huko kaskazini magharibi ya Tanzania, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Nje ya ubalozi wa Tanzania mjini Washington Jumatano, Kimambi alilitaja jina la rais wa kwanza wa Tanzania.
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ikiwa kuna kiongozi ambaye hafuati utawala wa sheria na kuheshimu katiba, ni jukumu letu kumdhibiti,” amesema. Hata kama ikimaanisha kuwa utalipa gharama kubwa kwa kukabiliana na hatari yoyote ile, bila ya kujali vitisho vinavyotolewa na utawala huo.”
Siku ya Jumanne, Kimambi alidai kuwa kupitia mtandao wake wa Instagram kuwa wawakilishi wa Shirika la Upelelezi wa Makosa ya Jinai (FBI) na Idara ya Polisi ya Los Angeles ilimfuata akiwa uwanja wa ndege Los Angeles, wakati akijitayarisha kupanda ndege , wakimtahadharisha juu ya usalama wake huko Washington.
Aliweka picha za business card za FBI na LAPD, zilizokuwa katika sehemu ya meza ndogo ya kwenye ndege, ikiwa na majina na namba za mawasiliano. Pia aliandika kuwa anatetemeka kutokana na vitisho hivyo.
Laura Eimiller, msemaji wa ofisi ya FBI Los Angeles, ameiambia VOA kuwa ni kinyume cha sera ya taasisi hiyo kuthibitisha au kuzungumzia iwapo FBI imefanya jambo kama hilo.
Kimambi alikuwa akimuunga mkono kwa nguvu zote Magufuli wakati wa uchaguzi mwaka 2015. Lakini, baada ya kuchukua madaraka, alimgeukia kwa hatua rais alizochukuwa kupiga marufuku vyama vya siasa kujishughulisha na siasa na kwa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za bunge.
No comments
Post a Comment