Followers

Tabia kuu ya wanaume wa Dar es Salaam haipendezi


Kama sio uchoyo na roho mbaya, basi huenda ni kweli Maisha ni magumu zaidi Dar es Salaam kuliko sehemu nyingie yeyote Tanzania kwa sababu wanaoishi huko wana aina yao ya maisha inayotofautiana kabisa na mikoa mingine kana kwamba Dar ni nchi tofauti na Arusha, Kigoma, Lindi na Pwani.

Wanaoishi Dar wanafahamu kuwa mikoani huwa kuna miezi 12 kwa mwaka, na mara nyingi ule mwezi wa mwisho wa mwaka unakuwa ni mwezi wa wao kutoka Dar kwenda kuwatembelea ndugu mikoani.

Yaani baada ya kutokomea mjini kwa kipindi kirefu, unaamua kwenda kumtembelea mdogo wako ukiwa na mke na watoto wako watatu.

Kwa sababu wewe ni ndugu yake kabisa, mdogo wako anaona kuna kila sababu ya kukupokea kifalme; anakufuata stendi, tena siyo peke yake, na mkewe na watoto wake. Mnashuka kwenye basi, wanawaona, wanawachukua kwa furaha na kwenda nanyi hadi wanapoishi. Mnapofika wanachukua mabegi yenu, wanayaingiza ndani, mtapumzika nao kidogo huku mkipiga stori za kukumbushana vitu mbalimbali kwa furaha na upendo uliozidi kipimo, lakini baadae kidogo, jua likizama, mnaandaliwa chakula kizuri cha jioni, mnakula pamoja na kuendeleza soga.

Usiku ukifika, muda wa kulala, shemeji yako anawaandilia kitanda; na anafanya hivi bila kusukumwa, anafanya kwa moyo safi na mkunjufu unaofurika upendo.

Asubuhi mkiamka ndiyo balaa, mnapigwa chai nzito kweli kweli. Mihogo ya kuchemsha, asali na nyama pembeni. Mnakula huku mkisifia jinsi mihogo inavyoiva vizuri.

Mtakaa huko kwa takriabni siku 20, kisha ndiyo mtapanga kurudi Dar es Salaam, na wakati mnarudi mnafungashiwa zawadi sio mchezo, hadi kwenye basi inawabidi mzilipie pia. Mnafika Dar mkiwa salama.

Inatokea siku, uko ofisini, unapokea simu ya kutoka kwa mdogo wako. Anakwambia; ‘Kaka, wiki ijayo nakuja kuwatembelea Dar es Salaam’.

Papo hapo moyo wako unaingia giza la ghafla, unamjibu sawa, karibu – lakini roho yako inasema sitaki hata kukuona, kwamba hujafurahishwa na mdogo wako kuja kukutembelea wiki ijayo.

Unarudi nyumbani unamuelezea mke wako hali halisi, tena unamuelezea kwa mtindo wa kumlaumu mdogo wako. Eti; ‘Yaani sijui wanafirikia Dar unakujakuja tu, mtu unashindwa kutoa taarifa muda mrefu, eti unanipigia simu wiki ijayo nakuja?’ – kweli kaka? Yaani ndugu yako kukutembelea unataka atoe taarifa mwaka mzima; hata wadogo zake Dk. Magufuli hawatoi taarifa namna hiyo wakitaka kuonana na kaka yao pale magogoni, kwanini iwe wewe?

Usiku mzima wewe na mke wako mnamjadili tu huyo mdogo wako, kwamba anakuja kuharibu bajeti eti kwa sababu mjini kila kitu ni pesa. Ni kweli anaharibu bajeti, lakini bajeti sio pesa tu, hata nyinyi mlivyokwenda kumtembela mliharibu bajeti yake – ile mihogo ya kuchemsha na asali mliyokula ingemsaidia yeye na familia yake siku za mbeleni.

Hivi kwanini turuhusu ugumu wa maisha uyayayushe upendo unaompendeza Mungu? Maisha magumu hayawezi kuisha hata uwe na pesa za dunia nzima, kamuulize Billgate kama huwa anafurahi muda wote. Tupendane tu.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.