UONGOZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umesema kuwa unajipanga kuhakikisha unaisaidia na Yanga katika mchezo wake wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolayta Dicha utakaofanyika Aprili 18, mwaka huu huko Ethiopia.
Lengo kubwa la TFF kufanya hivyo ni kutaka kuiona Yanga inatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo kwani ndiyo timu pekee iliyobakia msimu huu ambayo inaipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Katika mechi ya juzi Jumamosi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar er es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyoiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua hiyo ya makundi.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alisema kuwa ili kuhakikisha timu hiyo inasonga mbele katika michuano hiyo, wamejipanga vilivyo kuisaidia iweze kutimiza ndoto hiyo katika mechi ya marudiano.
“Tutaipatia muda wa kutosha wa maandalizi lakini pia tutatuma wawakilishi wetu Ethiopia kabla ya mechi hiyo kwa ajili ya kwenda kuweka mambo sawa ili siku itakapoenda huko isikumbane na usumbufu.
“Michuano hii ni ya kimataifa na ikifanya vizuri sifa itakuwa siyo kwa klabu pekee bali kwa taifa zima la Tanzania, kwa hiyo inatubidi tushirikiane nao kwa karibu kabisa ili kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo wake huo wa marudiano,” alisema Kidao.
No comments
Post a Comment