Wanakijiji wazika kipande cha utumbo na mguu wa mtoto aliyeliwa na fisi; MWANZA:
Mabaki ya mguu mmoja na kipande kidogo
cha utumbo wa anayeaminika kuwa mtoto wa miaka sita mkazi wa Mwaniko
wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Martha Saimon, aliyeliwa na fisi
yamezikwa leo kijiji hapo.
Martha, mwanafunzi huyo wa chekechea wa
Shule ya Msingi Mwaniko alikutwa na janga hilo alipokuwa amekwenda
kujisaidia akiwa na ndugu zake wawili baada ya kumaliza kula chakula cha
usiku, Aprili 25.
Bibi wa marehemu Kweji Samwel (52),
amesema wamefanya maziko ya mguu mmoja na kipande cha utumbo
vilivyopatikana baada ya msako mkali kuutafuta mwili na fisi huyo.
“Taratibu zote za maziko zimefanyika
kama kawaida licha ya kuwa tumezika baadhi ya viungo vyake tulivyopata.
Jambo hili limetuumiza kwa kiasi kikubwa,” amesema Kweji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hezron
Lutonja amesema kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji hicho ilikaa
na kujadili tukio hilo la aina yake ambalo halijawahi kutokea kijijini
hapo.
Amesema kamati hiyo imependekeza kuwaita
wawindaji wa kijadi wa wanyama hatarishi (Wama) kutoka Kijiji cha
Sumbugu wilaya hapo kwa ajili ya kuwawinda wanyama hao ili wasilete
athari zaidi.
No comments
Post a Comment