Followers

Hotuba upinzani mtandaoni



KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema leo inatarajia kutoa kile ilichokiita waraka kuhusu masuala yanayoihusu Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla.

Freeman Mbowe.

Ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara ya Habari na Elimu ya Bunge inaonyesha kuwa leo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, atawasilisha bungeni mjini hapa makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameshaweka wazi kwamba hapatakuwa na hotuba za upinzani katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, aliiambia Nipashe kuwa leo kutakuwa na hotuba ya upinzani.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa Arusha Mjini (Chadema) alisema hotuba hiyo haitasomwa bungeni bali itasambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Sisi hatusomi hotuba zetu bungeni tangu mkutano huu umeanza kama ilivyoelezwa na kiongozi wetu, Mheshimiwa Freeman Mbowe. Hatufanyi hivyo kwa sababu wamekuwa wakihariri na kuchuja hotuba zetu,” Lema alisema.

“Kama Bunge linafanya sensorship ya hotuba zetu maana serikali inataka tuandike wanachotaka wao. Na kazi ya upinzani ni kuandika chochote kiwe ni kizuri au kibaya kwa serikali, ndiyo ukosoaji wenyewe, tunawarekebisha na kuwashauri serikali.

“Kwa maana hiyo, tuliamua kama kambi kwamba hatutaweka hotuba zetu katika shughuli za Bunge. Lakini hotuba hiyo (ya leo ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) tumeiandaa.

“Tutaipeleka kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Waone mawazo yetu mbadala kama tungekuwa na fursa ya kuziweka kwenye hili Bunge la Bajeti.”

Pasi na kueleza kwa kina yaliyomo ndani ya waraka huo, Lema alisema kutakuwa na masuala yanayohusu uhusiano wa Jeshi la Polisi na raia wa kawaida na changamoto zinazolikabili jeshi hilo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla.

“Ina mambo mengi tu; ukatili wa Jeshi la Polisi, mambo mengi yanayoihusu Wizara ya Mambo ya Ndani. Ripoti hiyo ipo nitaiachia kesho (leo). Wakati wao wanasoma ya kwao, na mimi ya kwangu 'ta-release' (nitaiachia),” Lema alisema na kuongeza:

“Watu waone kwamba haya ndiyo yalikuwa mawazo yetu, lakini tungeyapeleka bungeni yangekataliwa. Tumeongelea mambo mengi sana, lakini hotuba yetu imejikita zaidi katika usalama wa raia na mali zao na mustakabali wa nchi yetu.

“Tumeongelea pia uhusiano wa askari polisi na raia na hata polisi wenyewe tumewatetea katika waraka wetu huo kwa kuzungumzia maslahi yao, wana changamoto ya nyumba za kuishi.

“Kwa miaka nane ambayo nimekuwa mbunge, bajeti ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ujumla haijawahi kutekelezwa kikamilifu. Polisi wana shida nyingi, si nyumba tu, hata sare ni shida na wakati mwingine wanakosa hadi magari kwa ajili ya shughuli zao. Yapo mambo mengi, kesho (leo) mtaona kwenye waraka wetu.”

Tangu kuanza kwa mkutano wa Bunge la Bajeti Aprili 3, upinzani hawajawahi kuwasilisha hotuba hata moja kama ilivyokuwa katika mikutano iliyopita kutokana na kile kilichoelezwa na Mbowe mwanzoni mwa mwezi uliopita kuwa mbali na mambo mengine, uongozi wa Bunge umekataa kuwaongeza mkataba wa ajira watendaji wanne wa sekretarieti ya upinzani ambao mikataba yao ya kazi ilifika kikomo Desemba mwaka jana. 

PAKUA[DOWNLOAD] SASA APPLICATION YA SUPERNIDA KUPATA HABARI ZOTE KILA SAA BONYEZA HAPA >>>>DOWNLOAD SASA BONYEZA HAPA.>>>>>

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.