Kesi ya billionea Msuya Utata Mtupu
MAELEZO ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya tanzanite, ‘Bilionea’ Erasto Msuya (43), yamezua mzozo mkali wa kisheria uliodumu kwa saa nne na nusu.
Mvutano huo wa kisheria uliibuka kutokana na hoja ya mawakili wa utetezi kudai kwamba maelezo hayo yamechezewa.
Utata huo unadaiwa kuwapo katika maelezo ya onyo ya Sharif Athuman ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya tanzanite na mchimbaji mdogo katika migodi ya Mirerani iliyoko Simanjiro, mkoani Manyara.
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, mwaka 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo ndiye aliyeibua mzozo huo jana, baada ya kudai kwamba wanazo hoja nne za pingamizi.“Mheshimiwa Jaji, tunaomba ku-iaddress (kuiarifu) korti kuhusu kile tulicho nacho, kabla ya kutoa mapingamizi yetu.
Nyaraka tuliyoonyeshwa leo hii kwamba ni ‘caution statement’ (maelezo ya onyo) awali wakati tukiwa kwenye mahakama yako tukufu niliomba kupatiwa nakala ya maelezo yaliyoandikwa kama onyo na mahakama yako ikatoa amri kwa Wakili Mkuu wa Serikali (Neema Mwanda) kutupatia na akaahidi atatupatia baada ya kutoa nakala.
“Baada ya kufanya hivyo, State Attorney (Wakili wa Serikali) Nyambita alimkabidhi mshtakiwa (Sharif) nakala halisi na mshtakiwa alinipatia.
Hii ya leo imejazwa sehemu ambazo nakala tuliyoipata kupitia kwa mshtakiwa na ambayo ilisomwa wakati wa ‘comital proceeding’ (kikao cha kufungasha ushahidi kwenda mahakama kuu) siyo ile.
Imejazwa tofauti na ile tuliyosomewa na kwa kuingalia, inaonyesha kuna utofauti wa mwandiko na hata rangi ya wino. Naomba mahakama yako imruhusu mshtakiwa (Sharif) athibitishe kama ndiyo hiyo aliyopewa na kuipokea kutoka kwa State Attorney (Wakili wa Serikali) Nyambita,”
Aliporuhusiwa kusimama, Sharif alidai kuwa Oktoba 9, 2015, yeye pamoja na washtakiwa wenzake katika kesi hiyo walipewa nakala hiyo ambayo yeye binafsi alimpatia nakala hiyo wakili wake, Ndusyepo.
Wakili Ndusyepo alidai mahakamani hapo kwamba mshtakiwa anakataa kwamba maelezo hayo ya onyo si yake, bali kwa kuwa alilazimishwa kutia saini maelezo ambayo yaliandikwa siku moja kabla ya kukamatwa kwake.
Baada ya uthibitisho huo wa mshtakiwa kukabidhiwa nakala, Wakili Ndusyepo aliiomba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi ikubali kumruhusu Wakili Majura Magafu kutoa sababu za pingamizi hizo.
Mosi; Wakili Magafu aliposimama alidai kwamba sababu ya kwanza ni maelezo hayo ya onyo kukosa uhalisia na jambo la pili ni uwezo wa shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi Damian Chilumba kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kukosa uwezo wa kutoa maelezo hayo kama kielelezo cha ushahidi mahakamani.
Tatu; shahidi huyo (Chilumba) hakukidhi vigezo kwa mujibu wa Kifungu cha 50 cha Kanuni za Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai ya Mwaka 2002, ambacho kinaelekeza mtuhumiwa anapokamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi, anatakiwa atoe maelezo yake ndani ya saa 24 tangu akamatwe.
“Nne ni rai yetu kwamba Kifungu cha 57 cha CPA (Kanuni za Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai) na ‘Declaration’ (uthibitisho wa Ofisa wa Polisi) inakinzana na maelezo yanayotolewa leo. Ukurasa wa kwanza wa ‘statement’ hii (maelezo) umekuwa ‘tempered with’ (umechezewa) kinyume cha ile ‘statement’ iliyotolewa wakati wa ‘comital proceeding’. Sehemu ya onyo ukurasa wa kwanza iliandikwa jina la mwandishi pekee ambaye yuko kizimbani, lakini sehemu nyingine zilikuwa hazijajazwa,” alidai Magafu.
Akijibu pingamizi hizo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalla Chavula alidai kuwa upande wa mashtaka haukubaliani na pingamizi hizo kwa vile hazina mashiko wala miguu ya kusimamia katika macho ya kisheria.
“Mheshimiwa Jaji, nianze na suala la uhalisia kwenye ‘caution statement’; hiyo ‘document’ (maelezo ya onyo) waliyo nayo hatuelewi imetoka wapi ingawa wenzetu wanasema kuna ‘serious criminal offence’, lakini sisi hatutaki tufike huko kama wanataka tufike na suala la mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo yake ndani ya saa 24, Tanzania tunayo sheria maalumu kwa hivyo hatuwezi kuishauri mahakama kujielekeza katika sheria ambazo hazijapitishwa na Bunge letu,” alidai Chavula.
Kuhusu madai ya kukiukwa kwa Kifungu cha 53 cha Kanuni ya Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai, Wakili Chavula aliiomba mahakama hiyo isikubali kutilia maanani hoja hizo za pingamizi kwa sababu kwa hatua hiyo mahakama haiwezi kufanya mlinganisho wa shahidi yupi anasema kweli kwa sasa na yule alisema hivi.
Baada ya kumalizika kwa mzozo huo wa kisheria, Jaji Salma Maghimbi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 2, mwaka huu atakapotoa uamuzi wake kuhusu utata uliojitokeza na kuibua pingamizi hizo.
Awali jana asubuhi, Jaji Maghimbi pia alitoa uamuzi kuhusu pingamizi lililotolewa wiki iliyopita kupinga kupokelewa kwa koti la kaki linalosadikiwa kuvaliwa na mmoja wa washtakiwa wakati wa kutekeleza mauaji ya Bilionea Msuya.
Katika uamuzi wake, Jaji huyo alisema mahakama yake imepima hoja zilizotolewa na upande wa utetezi na majibu yaliyotolewa na upande wa mashtaka katika kesi hiyo na kubaini kuwa kulikuwa hakuna mtiririko sahihi wa utunzaji wa kielelezo hicho tangu lilipokamatwa hadi kuhifadhiwa, hivyo anakataa kupokelewa kwa koti hilo lililotolewa na shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, Ispekta Chilumba.
Wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Saidi maarufu kama “Mredii” (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu.
Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, na Alli Musa maarufu “Majeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara. Kesi hiyo ya mauaji ya Bilionea Msuya ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Oktoba 4, 2015. Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Abdala Chavula, akisaidiwa na Kassim Nassir na Ignas Mwinuka.
Mawakili wanaounda jopo la utetezi katika kesi hiyo ni Hudson Ndusyepo anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tano, Emmanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshtakiwa wanne, sita na saba.
Hadi sasa, mashahidi 27 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao mahakamani hapo ambao ni kati ya mashahidi 51 waliopangwa na Jamhuri kuijenga kesi hiyo.
Kesi hiyo itaendelea tena Jumatano (kesho).
No comments
Post a Comment