Followers

Mbunge adai kufinywa makalio na kiti



HII sasa kali! Katika hali isiyo ya kawaida, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), amelalamika kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuhusu kile alichodai kufinywa makalio na kiti anachokalia bungeni mjini hapa.

Selasini ambaye ni mmoja wa waasisi wa mfumo wa vyama vingi nchini, aliyasema hayo bungeni jana, aliposimama na kumwomba Spika Ndugai kuagiza ufanyike ukarabati wa vifaa ndani ya Ukumbi wa Bunge hilo, akidai kuwa asilimia kubwa ya viti vimechakaa.

“Mheshimiwa Spika, inawezekana  watendaji wako kuna taarifa hawakupi kuhusiana na Bunge letu. Mheshimiwa Spika umri wetu kwa sasa ni hatarishi, viti kama vya kwangu hivi leo (jana) kimenifinya makalio,” Selasini alisema na kulilipua Bunge kwa shangwe.

“Ni lini Mheshimiwa Spika viti vitabadilishwa, ili wabunge waweze kufanya kazi zao katika hali ya amani na salama?” Selasini alihoji huku akicheka.

Akijibu mwongozo huo, Spika Ndugai alimwambia mbunge huyo kuwa suala hilo litafanyiwa kazi na ofisi yake.

“Kuna watu wanauliza eti ni sehemu gani umefinywa… usijali Mheshimiwa ‘point noted’,” alisema Ndugai kuwafanya watunga sheria wacheke zaidi bungeni.

Tangu Februari, Selasini ambaye wabunge wengi wamekuwa wakimwita Baba Paroko, amekuwa akihoji kuhusu ukarabati wa viti vya Bunge akieleza kuwa vingi vimechakaa na vimekuwa hatarishi kwa usalama wa wabunge.   

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.