‘Mjane wa Magufuli’ atoka jela kwa msamaha wa Rais
Tanga. Swabaha Shosi anayetambulika kwa jina la “Mjane wa Rais Magufuli” aliyehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela kwa kuingia bila kibali eneo la bomba la mafuta Chongoleani mkoani hapa, ameachiwa kwa msamaha wa Rais.
Swabaha, aliachiwa Jumamosi ya wiki iliyopita baada ya kupunguziwa adhabu hiyo kwa msamaha wa Rais alioutoa Aprili 26 katika maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Swabaha aliyejipatia umaarufu baada ya kujitokeza mbele ya Rais Magufuli katika moja ya mikutano yake, akimtaka Rais amsaidie baada ya kudhulumiwa nyumba ya marehemu mume wake.
Hata hivyo, wakati kesi yake ya mirathi ikiendelea Machi 29, Swabaha alifungwa jela miezi mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuingia eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta bila kibali.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alisema Swabaha alitoka gerezani Jumamosi jioni baada ya kufaidika na msamaha huo.
“Mfungwa namba 249/18 akiitwa Swabaha Shosi ametoka gereza la Maweni alikokuwa akitumikia kifungo cha mezi mitatu baada ya kufaidika na msamaha wa Rais wa robo, kosa lake halikuwa na kipingamizi cha kutopewa msamaha huo,” alisema Masunga.
Aprili 4, baada ya kuhukumiwa wakili wake, Obediodom Chanjarika aliwasilisha maombi ya rufaa mbele ya hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Hilda Lyatuu.
Maombi hayo ni rufaa ya kupinga hukumu iliyosababisha afungwe miezi mitatu na dhamana ya kuwa nje wakati akisubiri kusikilizwa kwa rufaa hiyo. Hata hivyo, Aprili 19, Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana, Swabaha alisema ataendelea na kesi yake ya kupinga hukumu hiyo ya miezi mitatu.
No comments
Post a Comment