Tanzania imekanusha ripoti mpya inayoishutumu serikali ya Tanzania na baadhi ya kampuni za kitalii na uwindaji kwa kuendelezwa kwa vitendo vya unyanyaswaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa watu wa jamii ya Kimaasai wanaoishi katika baadhi ya vijiji wilayani Loliondo.
Serikali ya Tanzania inasema tuhuma hizo ni "potofu" na kwamba zina lengo la kuipaka matope serikali ya Tanzania.
Katika ripoti hiyo, taasisi ya Oakland inadai kwamba, ukiukwaji huu wa haki za binaadamu unahusiana na mgogoro wa ardhi ambao umekuwepo kwa miaka mingi kati ya watu wa Jamii ya Kimaasai wanaopigania urithi wa ardhi yao na serikali kwa upande wingine inayodai kutaka kutunza ardhi hiyo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.
Ripoti hiyo yenye kurasa zaidi ya arobaini imesheheni shuhuda za watu wa jamii ya Wamaasai wanaoishi katika ardhi hiyo inayopiganiwa.
Watu hao wamewaambia watafiti wa ripoti hiyo kwamba serikali ya Tanzania imekuwa ikitumia sheria za uhifadhi kuwatoa kwa nguvu katika ardhi ya urithi kutoka kwa mababu zao.
Wameongeza pia kwamba, kampuni hizo za kitalii na uwindaji zimekuwa zikiwazuia kutumia vyanzo muhimu vya maji na kushutumu kampuni hizo kutumia polisi kuwapiga na kuwakamata.
Awali, kampuni mojawapo inayoshutumiwa iliwahi kuiambia BBC kwamba, wakati pekee ambao jamii hizi zinazuiliwa kuingia katika maeneo ya uwindaji kufikia vyanzo vya maji ni miezi kati ya Julai na Desemba ambao ni msimu wa uwindaji - kitu ambacho ni msimu wa upungufu wa maji pia.
Serikali kwa upande wake imekuwa ikikataa kuhusika na unyanyasaji wowote ule wa jamii hizi za Wamasai na kudai kwamba sheria za uhifadhi zilizopo zinalenga kutunza na kuendeleza tu maeneo ya uhifadhi na viumbe vilivyomo ndani ya maeneo hayo
No comments
Post a Comment