Wanahabari watakiwa kuwa macho kazini
Dodoma. Waandishi wa habari wametakiwa kuwa macho kazini hasa katika kipindi hiki ili kuepuka kuingia kwenye matatizo.
Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Ndimara Tegambwage alisema hayo jana alipokuwa akitoa mada katika kongamano kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari jijini Dodoma.
Amewataka waandishi wa habari kuendelea kuihoji Serikali kwenye mambo ya msingi bila woga lakini kwa kufuata misingi ya weledi bila kukandamiza upande mmoja kwa malengo ya kuuza habari.
“Mna wajibu pia wa kuikumbusha Serikali kuhusu yale mnayohoji na kama yametekelezwa ili kuhakikisha mnajenga misingi imara kwenye taaluma ya kuhoji mambo ya msingi ya maendeleo ya nchi,” alisema Tegambwage ambaye pia ni mhariri wa jamii wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).
Awali, makamu wa rais wa Klabu za Vyombo vya Habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanji alisema kuna wakati waandishi wa habari wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa uhuru kwa sababu ya kutishwa.
Alisema UTPC imekuwa ikisisitiza wakati wote kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.
Ndugai: Tukosoeni lakini...
Akifungua kongamano hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Bunge halikatai kukosolewa isipokuwa waandishi habari wanapofanya hivyo wafanye bila kutukanana na kudharauliana.
Baadhi ya waandishi wa habari wameitwa bungeni kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu machapisho yao kwenye vyombo vyao juu ya shughuli za mhimili huo wa dola.
Ndugai alisema, “Baadhi ya wabunge wangu na mimi tumekuwa waathirika wa jambo hili. Na wakati mwingine hata taarifa za Bunge zimekuwa hazitolewi kwa usahihi. Ni matarajio yangu kuwa kongamano kama hili litajaribu kuangalia namna gani ya kutenda kwa ubora zaidi kwa kuhakikisha kuwa habari zinazotoka zinakuwa ni habari za ukweli na uhakika.”
Spika alisema Bunge lina imani na waandishi wa habari na kuwataka kupendekeza jinsi gani wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na mhimili huo ili kusaidia ujenzi wa Taifa.
Alisema wapo wanaowafanya wabunge na viongozi wa Bunge kuwa kama hamnazo. “Waafrika tuna tatizo kidogo la kudharauliana kupita kiasi. Wakati mwingine huyo anayedhani hatuelewi tunachofanya kumbe yeye ndiye haelewi tunachokifanya.”
Alisema, “Wanaweza wakawa wamekosea lakini basi wakosolewe kwa kosa walilolifanya lakini si kuwafanya kama ni kundi la wajinga fulani, hapo ndipo penye shida ya baadhi ya waandishi wetu na vyombo vya habari.”
Ndugai alisema wote waliofika mbele ya kamati ya Bunge kuhojiwa kuhusu habari walizochapisha waliishia kuomba radhi kwa makosa waliyofanya.
Alisema utandawazi umeongeza fursa na kuwafanya wananchi kuwa kama wanahabari.
“Lakini mitandao hii imekuwa ikisambaza habari zisizo za ukweli na kuwapotosha sana wasomaji. Tunapokuwa tunajadili uhuru wa habari, hatuna budi kuangalia pia eneo hili la mtandao kwani ni chanzo kikubwacha maarifa lakini ni jukwaa kubwa la upotoshaji habari,” alisema.
Mwenyekiti wa taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa Tan), Salome Kitomari alisema wanatambua mchango wa Bunge hasa wa kutunga sheria.
“Ombi moja kwako ni kuwa sheria zinazotungwa na hasa zinazohusu kusimamia vyombo vya habari zihakikishe hazinyimi fursa ya vyombo hivyo kufanya kazi kwa uhuru kwa manufaa ya wananchi wote,” alisema.
Alisema baadhi ya kanuni za sheria zinazotungwa na mamlaka zilizopewa nguvu na sheria zinakiuka baadhi ya haki za msingi ambazo wakati mwingine zinatolewa na sheria mama zinazotungwa na Bunge, hivyo kuwanyima wananchi haki ikiwamo ya uhuru wa mawazo na kujieleza.
Akizungumzia hofu kwa waandishi wa habari, Salome alisema kupotea kwa mwanahabari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda tangu Novemba 21, mwaka jana kumechangia hofu hiyo.
“Vitisho kwa wanahabari na kufungiwa kwa baadhi ya magazeti. Haya yataendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na kwa nafasi yenu, tunaomba muendelee kuyakemea,” alisema.
No comments
Post a Comment