Maria na Consalata: Pacha walioungana Tanzania waliowagusa wengi wafariki dunia
Maria na Consolata, pacha waliozaliwa wakiwa wameungana nchini Tanzania na wakaishi hadi kujiunga na chuo kikuu wakiwa bado wameungana, wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Pacha hao walifariki dunia wakiwa katika hospitali ya Iringa.
Kifo chao kimewagusa wengi Tanzania, wengi wakituma salamu zao za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli, ambaye miezi kadha alikutana na pacha hao, ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vyao.
"Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa," ameandika Rais Magufuli kwenye Twitter.
Pacha hao waliokuwa na umri wa miaka 22 wamekuwa wakitunzwa na watawa wa kanisa Katoliki tangu baada ya kuzaliwa.
Mwaka jana, walijiunga na chuo kikuu cha Ruaha Catholic University na kuanza na masomo ya kompyuta kabla ya kuanza masomo kamili Oktoba.
Maria na Consolata walikuwa wamefanya mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa, Kusini magharibi mwa Tanzania na kufaulu.
Maisha ya Maria na Consolata
Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa eneo la Ikonda, wilaya ya Makete kusini magharibi mwa Tanzania mwaka 1996.
Walisoma shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye wakasomea hadi kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilaya ya Kilolo.
Septemba mwaka jana, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walijiunga na chuo kikuu cha kikatoliki cha Ruaha, Iringa.
Walianza kuugua maradhi ya moyo na Desemba wakahamishiwa taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili.
Wamekuwa wakitatizwa na afya tangu wakati huo.
Walipofaulu mtihani wa kidato cha sita, walieleza furaha yao kuu baada ya kufaulu mtihani na kueleza ndoto zao.
"Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana," alieleza Consolata.
Walieleza sababu za kuchagua chuo cha Ruaha kwenye mkoa waliokuwa wanaishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao hupenda kubadili mazingira.
"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.''
Maria na Consolata walikuwa wamewahimiza wazazi kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu wakisema hakuna lisilowezekana.
"Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.''
No comments
Post a Comment