Benki yatoa msaada wa Vitanda maalum vya kuchangia damu
BENKI ya NMB imetoa msaada wa vitanda maalum vya kuchangia damu vyenye thamani ya Sh. milioni nane pamoja na kuchangia damu zaidi ya chupa 250 katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila.
Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, alisema kuwa wafanyakazi wameamua kujitolea fedha zao na kusaidia vifaa vya kutolea damu na wao kushiriki utoaji wa damu, ili kunusuru wagonjwa ambao wanahitaji huduma hiyo hospitalini hapo.
“Wafanyakazi hawa wamejitolea michango na kufanikisha kununua vitanda 10 maalum kwa ajili ya kuchangia damu vyenye thamani ya Sh. milioni nane,” alisema.
Alisema wamekuwa wakijitoa mara kwa mara kwa mambo mengine, lakini safari hii wameamua kuchangia eneo hilo la damu ili kusaidia kuokoa maisha ya wahitaji.
“Utaratibu wa kurejesha sehemu ya mapato kwa wateja umekuwa ukifanywa pia na Benki kwa kujipangia kutoa asilimia moja ya faida baada ya kodi kila mwaka na kuirejesha kwa jamii kupitia misaada kwenye sekta ya elimu na afya,” alisema.
Meneja wa Kitengo cha Uwabikaji kwa Jamii (CSR) cha benki hiyo, Lilian Kisamba, alisema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa wafanyakazi wa benki hiyo kwa kushirikiana na kitengo hicho kusaidia jamii yenye uhitaji.
“Wafanyakazi wamekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii kupitia programu ya ‘staff initiative" ambao ni mpango uliowekwa na kitengo cha uwajibikaji ili kusaidia matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili jamii,” alisema.
Pia alisema wafanyakazi wa Kanda ya Mashariki wakisaidiana na kitengo hicho walichangia Sh. milioni 13, ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa Hospitali ya CCBRT ili kufanikisha upasuaji wa kinamama wenye fistula.
No comments
Post a Comment