Fei Toto atibua usajili Yanga
Kutua kwa viungo wapya wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mohamed Issa ‘Banka’ kumemzuia kiungo wa Mtibwa Sugar, Salum Kihimbwa kutua Jangwani katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Kihimbwa ni kati ya wachezaji waliokuwepo kwenye mipango ya usajili ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Yanga hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kuwasajili wachezaji sita pekee ambao ni Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Jaffary Mohamed, Heritier Makambo, Fei Toto na Banka.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, imepata Yanga imemuondoa kiungo huyo katika mipango yao ya usajili ni baada ya kukamilisha idadi ya viungo aliyokuwa akihitaji kocha mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera.
Mtoa taarifa huyo alisema, usajili wao wanaoufanya unatokana na mapendekezo ya kocha mwenyewe katika ripoti ambayo ameikabidhi kwenye kamati ya usajili ya timu hiyo.
“Kihimbwa kwa sasa tumemuweka pembeni na badala yake tunaelekeza usajili wetu katika nafasi nyingine ambazo tumepanga kuziboresha ikiwemo safu ya ushambuliaji na ulinzi beki wa kati.
“Juzi tu tulisajili viungo wanne wapya ambao ni Fei Toto, Kaseke, Ngassa na Banka achana na wale wa zamani wenye mikataba, hivyo utaona tuna idadi kubwa ya viungo katika timu.
“Hatutaki kufanya usajili wa hovyo kama wa wale watani wetu, sisi usajili wetu tunaufanya kwa kufuata ripoti ya kocha ambayo ameitoa kwa uongozi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, kuzungumzia hilo alisema: “Kama uongozi wa Yanga tulifanya na tunafanya mazungumzo na baadhi wachezaji kwa siri kubwa kwa hofu ya wapinzani wetu kutuzidi katika usajili.
“Hivyo, mipango ya kumsajili Kihimbwa hata kama ilikuwepo nisingeweza kuweka wazi muda huu, kikubwa tusubirie kama atasajiliwa basi tutasema,”alisema Nyika.
No comments
Post a Comment