Kama Unataka Kufanikisha Malengo Yako, Fanya Zoezi Hili Kila Siku
Wataalamu wengi wa mafanikio wanasisitiza sana umuhimu wa kupitia malengo yako kila siku ili iwe rahisi kwako kuweza kuyatimiza. Unajua ni kwa nini hili linasisitizwa sana? Umeshawahi kujiuliza kwa nini?
Hiyo yote ni kuufanya ubongo wako uamini kwamba malengo yako yanawezekana. Hiyo iko hivyo pia kwa sababu kabla hujafikisha miaka mitano unakuwa umekataliwa mara 40,000 kwa vitu tofauti na ni mara 5000 tu ndio unakuwa umekubaliwa.
Mpaka hapo unaona kama umekataliwa mara nyingi hivyo, tafsiri yake ni rahisi kuona kila kitu hakiwezekani. Ili mambo hayo yawezekane sasa, inabidi uushawishi ubongo wako kuamini kwamba inawezekana.
Kumbuka mafanikio yanaanza na sisi wenyewe kwanza, yaani zile imani tulizonazo ndani mwetu, ndizo zinajenga mafanikio. Hivyo unatakiwa kujilisha vitu chanya na kujiaminisha kwamba inawezekana kwa lolote lile kwako, pitia malengo yako kila siku utafanikiwa.
Pitia malengo yako kila siku.
Hata kama kuna malengo umejiwekea na unataka uyafikie, lakini kila ukifikiria unaona malengo hayo ni makubwa sana kama hayafikiki hivi, kitu cha kufanya kwanza ili uyafikie malengo hayo, yapitie kila siku na acha kufikiria ukubwa wa malengo hayo, badala yake fikiria jinsi utakavyoanza kutekeleza malengo hayo.
Fikiria pale utakapoweka miguu yako kwa mara ya kwanza ili uanze utekelezaji wa malengo yako. Tafuta jinsi utakavyoanza kwanza. Kumbuka hata safari yoyote ndefu inaanza na hatua moja, hata malengo yako ili yatimie, litafute eneo utakaloweka miguu yako kwanza, na kisha kuendelea na utekelezaji.
Fanya zoezi hili la kupitia malengo yako kila siku na kila wakati, litakupa nguvu ya kuweza kusonga mbele na hadi kufikia mafanikio yako.
No comments
Post a Comment