Naibu Waziri wa Mali Asili na Utalii ametoa maagizo makali kwa TFS Songwe
Install Application hii ya supernida ili Upate Habari Kwa urahisi zaidi Bonyeza Hapa
NA Manuel Kaminyoge,Songwe,
Naibu Waziri Maliasili na Utalii Japhet Hasunga amestushwa na kasi ya ukataji miti katika eneo la chanzo cha maji yanayotumika katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe, kwa ajili ya kuchoma mkaa kisha kuagiza Wakala wa Hifadhi ya misitu kuanza mchakato wa kulifanya eneo hilo kuwa hifadhi ya Taifa na kuweka mizinga ya Nyuki.
Naibu Waziri huyo akiwa katika ziara ya kawaida katika Jimbo lake la Vwawa ameamua kutembelea chanzo hicho katika kata ya Nyimbili ili kuona uwezekano wa kuongeza vyanzo vingine kukisaidia ili kuongeza kiwango cha maji yanayotumika katika mji wa Vwawa ndipo alipokuta miti imekatwa muda mfupi uliopita.
Akizungumzia hali hiyo Mbunge huyo aliagiza Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Mbozi kufanya mchakato wa kulihifadhi eneo hilo kisheria ili kunusuru kukauka kwa vyanzo hivyo ambavyo vipo zaidi ya vinne katika safu za milima Ilengo.
“ kwa kweli hali inatisha hapa ninaona umuhimu wa kuzuia mkaa lakini lazima tuchukue hatua za kulidhibiti eneo hili ili liendelee kutoa maji na kusaidia kuvuta mvua kwa ajili ya maisha ya watu wetu na viumbe hai wanaotegemea chanzo hiki” amesema Hasunga.
Diwani wa kata ya Nyimbili Tinson Nzunda amesema jitihada kubwa inafanywa kulinda misitu katika eneo hilo lakini inaonesha kwamba wapo baadhi ya watendaji wa halmashauri ambao wanakula njama na waharifu na kufanya kazi ya uhifadhi kutokuwa na mafanikio.
“ tunatambua kwamba kuna watumishi wasio waaminifu katika eneo hili ambao wanaturudisha nyuma tunahitajika kuchukua hatua vinginevyo wataendelea kutusumbua” amesema Nzunda
Mkaazi wa Nyimbili Neema Mwashilindi amesema tabia ya ukataji miti inayofanywa na baadhi ya watu hasa wanaume kwa ajili ya kuchoma mkaa ili kujipatia kipato na wengine kwa ajili ya kuanzisha mashamba hivyo kuhatarisha mazingira ya eneo hilo na kuwa inahitajika elimu zaidi ili kila mmoja ajue umuhimu wa miti.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbozi ambaye pia ni Afisa Misitu Zakayo Mwamahonje amesema eneo hilo limekuwa likiwasumbua muda mrefu ambapo maofisa wake wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara mchana na usiku lakini bado kila wanapopita wanakuta uharibifu unaendelea.
Aidha eneo la safu ya milima katika kata ya Nyimbili ambalo ndilo hifadhi ya vyanzo vya maji vya Ilengo, Nalabha na vyanzo vingine ambavyo vinatarajia kutegwa maji kwa ajili ya matumizi ya mji wa Vwawa ambao ndiyo makao makuu ya mkoa wa Songwe, lakini eneo hilo wakazi wake hawanufaiki na maji hayo jambo ambalo linaweza kuwa chanzo cha ukataji miti unaoendelea.
Install Application hii ya supernida ili Upate Habari Kwa urahisi zaidi Bonyeza Hapa
No comments
Post a Comment