Followers

Rais Magufuli ajadiliana na Viongozi wastaafu Kuhusu hali ya nchi

Rais John Magufuli amewakaribisha viongozi wakuu wastaafu Ikulu huku akisema anajisikia mwenye baraka na heshima kubwa kukutana na viongozi hao.

Akizungumza leo Julai 3 katika hafla hiyo maalum, Rais Magufuli amesema amewakaribisha Ikulu ili ajadiliane nao kuhusu hali ya nchi na wamweleze bayana yale waliyoona ametekeleza vizuri na kumshauri pale alipoteleza.

Akiwakaribisha viongozi hao, Rais Magufuli aliyekuwa ameambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi amewataka viongozi hao wajisikie wapo nyumbani na wasiwe na hofu kuzungumza chochote wanachofikiria.

“Kwangu ni heshima kubwa kukutana nanyi leo, mmenipa heshima kubwa kuitika wito wangu na kuja hapa wengi wenu mmeacha kazi zenu. Naona furaha kwani viongozi wengi sijawahi kuonana nao tangu wastaafu au niingie madarakani. Namwona Jaji Samatta ...sijawahi kuonana naye tangu astaafu. Wengi sijawahi kuona nao baadhi yao nimekuwa nikiwateua tu nasaini kwenye makaratasi nikiamini ninawajua lakini sijawahi kuwaona. Mzee Lowassa amewahi kuja hapa Ikulu tulikutana naye,” alisema.

Amesema amewaita kujadiliana nao kwa vile wao ni viongozi muhimu na kwa nyakati tofauti walitoa mchango mkubwa katika taifa hivyo kwake ni jambo jema kuonana nao ili kujadiliana kuhusu mambo ya nchi.

“Nina bahati kuwa kuwa kiongozi wakati viongozi wengi wakiwa bado hai, ni sehemu chache duniani kuwa kiongozi halafu wale waliokutangulia wakiwa bado wapo, nashukuru sana,” alisema.

Viongozi anaokutana nao ni pamoja marais waastafu, akiwamo Benjamin Mkapa na Aman Karume. Pia yupo makamu wa rais mstaafu Mohammed Gharib Bilal. Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, Cleopa Msuya, John Malecela, Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.

Pia, wamo maspika wastaafu, majaji wakuu wastaafu na viongozi wengine waandamizi waliomaliza muda wao.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.