Yanga wagomea mazoezi, Kocha asema haya
Install Application hii ya supernida ili Upate Habari Kwaurahisi zaidi Bonyeza Hapa
MJUMBE wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Khalfan Kigwenembe amejiuzulu nafasi yake kutokana na mwenendo mbovu wa timu lakini na wachezaji nao wamegoma tena.
Kocha Mwinyi Zahera jana alikwenda mazoezini kwenye Uwanja wa Polisi Kurasini akajikuta yuko mwenyewe baada ya wachezaji wote kuendelea na mgomo ambao hata yeye haelewi chanzo.
Juzi Ijumaa alifika uwanjani hapo akakutana na wachezaji wapya tu lakini jana alipokwenda hata wale wapya hakuwakuta. Alipoulizwa na Spoti Xtra akasema ; “Leo ndio kabisa hawakufika hata mmoja. Nimeamua kuitisha kikao cha dharura na viongozi.”
Mmoja wa wachezaji wa Yanga alidokeza jana kwamba wameamua kususa ili walipwe malimbikizo yao ya mishahara na vilevile waelewe hatma yao klabu hapo kwani mambo yanakwenda mrama.
Yanga imepangwa kurudiana na Gormahia Ijumaa ijayo kwenye mechi za Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, lakini Zahera anasema haoni dalili yoyote ya ushindi wala kuepuka kipigo.
Uongozi wa Yanga licha ya kwamba hakuna aliyekuwa tayari kutoa ufafanuzi jana lakini inadaiwa kwamba wamechanganyikiwa na hawaelewi ni wapi watapata mkwanja wa kuokoa jahazi hilo huku siku za usajili zikizidi kuyeyuka
Zahera ambaye hapendi mzaha kazini, jana alikuwa na kikao kirefu na baadhi ya viongozi kujua nini kinachoendelea na wao wamechukua hatua gani baada ya wachezaji kususa mazoezi.
“Nimekaa na viongozi nimewaambia kila kitu wamesema watawaita wachezaji wazungumze nao, nasubiri kusikia kutoka kwao Jumatatu wakisusa tena nitatoa uamuzi wangu,”amesisitiza Zahera ambaye makazi yake yako ufukweni.
No comments
Post a Comment