Followers

Mambo muhimu ya kufanya unapoamua kuacha kazi


Umewahi kufikiria kuacha kazi? Haya si maamuzi madogo hata kidogo. Hata hivyo, zipo sababu kadhaa zinazoweza kukufanya uamue kuacha kazi. Mosi, kupata kazi mpya.

Unapoitwa kuanza rasmi kazi uliyoomba, ni vigumu kuendelea na kazi uliyonayo. Kwa kuwa ni vigumu kuwa na ajira mbili kwa wakati moja, mara nyingi utalazimika kuacha kazi uliyonayo.

Lakini pia inawezekana umechoka kuendelea na kazi uliyonayo kwa hiari yako.

Labda ni matatizo na mazingira ya kazi, mgogoro na mwajiri wako au mahusiano mabaya na wafanyakazi wenzako.

Kwa sababu yoyote ile inayokufanya uache kazi, ni muhimu kufanya maamuzi pasipokukurupuka. Hasira au hata furaha isiyo na kiasi isikufanye usahau kutafuta ushauri wa kitaalam utakaokusaidia kufikia maamuzi kwa kufuata taratibu rasmi.

Wapo wafanyakazi ambao, mara baada tu ya kupata kazi nzuri kwingineko, waliwaacha waajiri wao kwa dharau na mbwembwe.

Wengine waliacha kazi kwa notisi ya masaa 24 kwa kuamini hawana cha kupoteza tena. Mambo hayakwenda kama walivyofikiri na waliishia kujuta.

Fuata utaratibu

Kuna faida ya kuacha kazi kwa kufuata taratibu rasmi. Kwanza, inakusaidia kudai haki zako unazostahili kwa mujibu wa sheria. Ili uweze kupata haki zako, ikiwa ni pamoja na mafao yoyote unayostahili kwa mujibu wa mkataba wa kazi, zitahitajika nyaraka rasmi kuthibitisha uliacha kazi.

Aidha, kuheshimu mkataba kunakuepusha na uwezekano wa kujiingiza kwenye matatizo baada ya kuondoka. Unapoondoka kienyeji, mwajiri mkorofi anaweza kukuhesabu kuwa mtoro kazini na kukubebesha tuhuma za kuiba mali za ofisi zilizokuwa chini ya uangalizi wako.

Ondoka kazini kwa namna inayolinda mahusiano yako ya kikazi na mwajiri. Unaweza usilione hilo leo kwa sababu ya hasira au matumaini makubwa uliyonayo lakini baadae uhusiano mbaya na mwajiri unayeachana naye ukakugharimu.

Katika makala haya tunapendekeza namna nzuri ya kutoa taarifa ya kuacha kazi kwa mwajiri wako wa sasa na wafanyakazi wenzako.

Kutoa taarifa rasmi kwa mwajiri

Baada ya kujiridhisha kuwa umezingatia taratibu za kuacha kazi kwa mujibu wa mkataba, hatua inayofuata ni kufanya mawasiliano rasmi na mwajiri kuwa sasa unaacha kazi.

Si waajiri wengi wanaweza kufurahia kukutana na tetesi za mfanyakazi kuacha kazi ‘koridoni’ au kwenye vikao vya chai.

Epuka kueneza taarifa hizo kabla hujawasiliana rasmi na mwajiri.

Taarifa rasmi ya kuacha kazi ni muhimu, kama inawezekana, itanguliwe na mazungumzo ya ana kwa ana na mwajiri.

Katika mazungumzo hayo, mwajiri wako anapata nafasi ya kuzipokea habari mbaya katika mazingira yasiyo rasmi kabla hajasoma barua rasmi.

Katika kuandika barua ya kuacha kazi, yapo mambo kadhaa ya kuzingatia. Mosi, ni kuweka wazi kuwa nia yako kuwa unaacha kazi. Kwa mfano, barua yako inaweza kuwa na kichwa cha habari kinachosema, ‘RE: RESIGNATION’, ‘YAH: Kuacha kazi’ maneno kama, ‘kuhama kazi’, ‘kuchoka na mazingira ya kazi’, ‘kubadili kazi,’ yanaweza kuwa na tafsiri nyingi. Epuka maneno yenye tafsiri nyingi.

Baada ya kuainisha lengo la barua yako, andika sentensi inayotaja tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako. Mfano, ‘Ninakuarifu kuwa baada ya kutafakari kwa kina, kwa hiari yangu, nimeamua kufanya maamuzi ya kuacha kazi ili kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo.

Siku ya mwisho kufanya kazi inategemewa kuwa Jumatano ya tarehe 28/2/2018.’

Baada ya kutaja siku ya mwisho kufanya kazi, shukuru kwa kutambua mchango wa mwajiri wako katika kuboresha ujuzi wako. Taja kwa ufupi fursa ulizopata tangu umeanza kazi unazoamini zilizokujenga kiweledi na kiuzoefu.

Inawezekana kweli kuna mambo hukuyapenda katika kampuni/taasisi unayoondoka. Labda ulikuwa na mgogoro na mkubwa wako wa kazi.

Huu si wakati wa kulalamika wala kukumbushia maumivu yaliyopita. Tumia lugha chanya isiyoonyesha hisia hasi.

Sambamba na hilo, epuka kumtaja mwajiri wako mpya wala unakokusudia kwenda. Mwajiri haitaji kujua mipango yako baada ya kuachana naye.

Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi.

Unaweza pia kuonyesha uko tayari kwa usaili wa kuacha kazi kumpa fursa mwajiri kukudadisi sababu zilizokufanya uondoke; namna utakavyopewa haki zako; utaratibu wa makabidhiano ya ofisi; utayari wako katika kumsaidia mtu mpya atakayepatikana kuchukua nafasi yako na mambo kama hayo.

Kuwajulisha wafanyakazi wenzako

Baada ya makubaliano rasmi na mwajiri wako kwamba sasa unaacha kazi, kinachofuata ni kuwajulisha wafanyakazi wenzako. Hawa ni watu uliofanya nao kazi na mmekuwa na mahusiano ya karibu.

Taarifa kuwa sasa unaondoka zinaweza kuibua hisia za wivu. Unapowajulisha, heshimu hisia zao.

Ni kweli umeacha kazi na unakwenda mahali bora zaidi. Pengine hata wafanyakazi wenzako wangependa kwenda huko unakokwenda wewe.

Usiwafanye wajione hawana mahali pa kwenda kwa kuendelea kubaki na mwajiri unayeachana naye.

Ukifanya hivyo, unaharibu uhusiano na watu wanaoweza kuwa sehemu muhimu ya mtandao wako wa kazi na ajira.

Huna sababu ya kufanya majigambo ya maneno na vitendo kabla na baada ya kuondoka kwenye kituo cha kazi.

Hakuna sababu ya msingi kueleza kwa nini umeondoka na kwamba unakokwenda kuna maslahi zaidi. Kama ni mafanikio uliyonayo na unayoyatarajia, waache wao wenyewe wayaone.

Kadhalika, usihatarishe uhusiano wako na mwajiri unayemwacha kwa kumsema vibaya kwa wafanyakazi unaowaacha.

Hata kama ni kweli ana mapungufu yake; hata kama mazingira hayo ya kazi unayoyaacha hayafai; huna sababu ya kuyaeleza hayo kwa wafanyakazi unaowaacha.

Sema maneno chanya.

Toa sababu za kawaida kwa nini unaondoka. Ondoka kwa namna ambayo itakufanya uendelee kuwa na mahusiano mazuri na hao unaowaacha. Kuna kesho.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.