Namna bora ya kumwandaa mtoto kufikia mafanikio na kutimiza ndoto
KATI ya mambo ambayo wazazi hukosea ni kutotengeneza mazingira mazuri ya watoto kufikia mafanikio na kutimiza ndoto zao.
Wazazi na walezi katika nchi nyingi, hasa zinazoendelea, wamekuwa wakiamini kuwa mafanikio ya watoto wao kimaisha yanatokana na bahati. Hii imesababisha watoto kukosa misingi mizuri na mwelekeo unaofaa katika uchaguzi wa fani na kuziishi ndoto zao.
Hebu jiulize maswali haya; hicho unachofanya sasa ndicho ulichotamani kukifanya ulipokuwa mdogo? Na je, unakifurahia?
Kuna uwezekano mkubwa majibu ya maswali haya yote yakawa hapana na sababu kubwa ni kuwa ulikosa mazingira wezeshi ya kufikia ndoto zako na matokeo yake umejikuta ni mhasibu mwenye sifa za mwanasheria.
Kizazi cha sasa hakitakiwi kuyapitia makosa yaliyofanywa na kizazi kilichopita, hivyo ni vyema kuhakikisha watoto wanatengenezewa mazingira wezeshi ya kufanya yale wanayoyatamani na kuyafurahia.
Mambo yafuatayo yanaweza kumsaidia mtoto kufikia ndoto zake na kuja kufurahia kile atakachokifanya baadaye;-
RAHISISHA UPATIKANAJI WA TAARIFA
Katika umri mdogo ni vigumu kwa mtoto kufanya uamuzi ya moja kwa moja. Mtoto hawezi kukwambia anapenda kuwa mwanasheria kama hafahamu wanasheria wanafanya nini.
Tulivyokuwa wadogo wengi tulikuwa tunapenda kuwa madereva na walimu na kwa wale waliokuwa na wazazi wafanyakazi, walitamani kufanya kazi walizokuwa wakifanya wazazi wao. Hii inatoa picha kuwa tulikosa taarifa juu ya fani nyingine zaidi ya zile zilizokuwa kwenye mazingira yetu.
Kwa mantiki hiyo, hakikisha unarahisisha upatikanaji wa taarifa juu ya fani mbali mbali ili mtoto awe na machaguo mengi.
Ongea na mwanao katika umri mdogo juu ya fani mbalimbali. Mwambie nani ni nani na anafanya nini. Hii itatanua mtazamo wake ambao mara nyingi umefungwa na mazingira yanayomzunguka.
CHUNGUZA MWANAO ANAPENDA NINI
Taarifa atakazopata mwanao juu ya fani, zitamfanya ajikute anapenda kitu fulani zaidi ya kingine. Hii inaweza kuonekana kupitia anachosema na anachofanya pia.
Wakati mwingine itakubidi uchukue muda kumwuliza na kumsikiliza kile anachopenda kufanya. Wakati mwingine inaweza kukuchanganya kwa kugundua kuwa pengine anapenda zaidi ya kitu kimoja. Bado hizo ni taarifa muhimu sana katika kufahamu nini anapenda kufanya.
TENGENEZA MAZINGIRA WEZESHI
Kipawa ni kama mbegu. Kinahitaji mazingira fulani ili kuchipua na kumea vizuri. Vitabu anavyosoma, video anazoangalia, watu anaokutana nao, mazungumzo unayozungumza nae ni sehemu ya mazingira muhimu ya kumuandaa katika fani fulani.
Ndoto za watoto zinaweza badilika kadri wanavozidi kukua, bado unajukumu la kuendelea kumtengenezea mazingira wezeshi ya kile anachokitaka.
EPUKA KUTAKA AFANANE NA WEWE
Moja ya makosa wanayoyafanya wazazi na walezi wengi ni kutaka watoto wawe kama wao. Wako wazazi ambao kama wao ni wahasibu wanatamani watoto wao wawe hivyo.
Kufanya hivyo ni kulazimisha mambo kusiko na ulazima. Hii itaishia kwa mtoto kufanya kitu asichokipenda na asichokifurahia pia. Kila mtoto anakuja na uwezo na vipaumbele vyake ambavyo vinaweza visifanane na vyako kabisa.
Ukimlazimisha mtoto mwenye mwelekeo wa kitangazaji kuwa mchungaji kwa sababu tu wewe ni mchungaji, jua unatengeneza mchungaji wa ajabu. Acha mtoto afanye kile kinachompa amani na furaha.
MTAFUTIE MSHAURI
Ukweli ni kwamba si kila kitu mtoto atakachohitaji kukifahamu utakuwa na taarifa nacho. Wako watu wenye uwezo mzuri wa kusoma tabia za mtoto na kumwelewa na pia kumshauri juu ya mambo yahusuyo fani anayopendelea au anazopendelea.
Kama mtoto ameonyesha nia ya kuwa daktari, tafuta mtu katika fani hiyo asaidie kumpa taarifa sahihi na kumtia moyo juu ya fani hiyo.
MJENGEE KUJIAMINI
Hakuna fani inayohitaji mtu mwoga, mwenye aibu na asiyeweza hata kusimama mbele za watu kuzungumza.
Kukosa ujasiri imekuwa ni moja ya sababu zinazo wafanya vijana wengi wahangaike kutafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio kwa sababu ni moja ya vigezo muhimu.
Ruhusu mwanao ajifunze lugha, achangamane na wenzake na ashiriki katika michezo mbalimbali. Fani yoyote ile inahitaji watu hodari wanaojiamini.
Ni vyema pia kumruhusu mtoto kufanya vitu vipya bila kuogopa kukosea na kusemwa vibaya. Pamoja na kumjengea kujiamini, pia itamwongezea mtoto ubunifu ambao pia ni muhimu katika fani nyingi.
MTIE MOYO NA KUMJENGEA UWEZO
Watu wengi hukata tamaa kirahisi pale watu wao wa karibu wanapokuwa sababu ya wao kukata tamaa na kurudi nyuma.
Watoto wanahitaji kusikia kutoka kwako ukiwaambia maneno ya faraja; inawezekana, utakuja kuwa mwalimu mzuri sana na maneno mengine ni muhimu katika kuchochea uwezo wa mwanao.
Pamoja na hayo, hakikisha mwanao anapata muda wa kujifunza. Mwandalie mazingira ambayo yataondoa vikwazo katika kupata elimu bora itakayo muwezesha kufikia malengo yake.
No comments
Post a Comment