Followers

Ndugulile awaasa wananchi kutoa taarifa wanapokosa matibabu


Na.Ahmad Mmow, Nachingwea.\
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto ,Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) amewaasa wananchi  kutoa taarifa pale watakapokwenda hospitali na kukosa matibabu kwasababu ya kukosekana dawa.

Ndugulile ametoa rai hiyo jana katika kijiji cha Naipanga,wilaya ya Nachingwea wakati wa kilele cha  kampeni ya kupima kwa hiyari maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambayo imepewà na kutambulika kwa  jina la  "Furaha Yangu ".

Aliwahakikishia wananchi hao na wengine wote hapa nchini kwamba serikali ya awamu ya tano haitaki kuona wananchi wakienda kununua dawa madukani hivyo imejipanga kuhakikisha dawa zote zinazotolewa na serikali zinawafikia.

Alisema katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa wananchi Serikali imewapeleka watumishi wa idara ya afya 48 katika wilaya hiyo ili wakatoe huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humu.

 "Upimaji wa virusi vya  UKIMWI ni mpango wa kitaifa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapima na kutambua afya yake, lengo ni  kuwafikia asilimia 90 ya watu walioambukizwa  na kutoa dawa,"alisema DkNdugulile ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kigamboni.

Kwa upande wake ,mkuu wa  wilaya Nachingwea, Rukia Muwango alisema zoezi la upimaji afya  katika wilaya hiyo ni endelevu, kwani umuhimu wa wananchi kupima na kutambua afya zao ni mkubwa huku akiweka wazi kwamba maendeleo yatatokana na uimara wa afya za wananchi kwasababu mtaji wa kwanza wa maendeleo na uchumi wa taifa ni afya.

Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kwamba kampeni  hiyo ya upimaji kwa hiari inayoendelea wilayani humo ambayo yeye kwa kushirikiana na watalaam wa idara ya afya anaratibu na kusimamia.Tayari wanawake 809 na wanaume 531wamejitokeza na kupimwa.

 "Hadi sasa miongoni mwahao waliopima ni watu saba  tu ndio waliokutwa na maambukizi ya VVU na wameshapata ushauri nasaha na kuanzishiwa dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya UKIMWI,"alisema Muwango.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.