Followers

Ninapoiona Bongo Movie iliyo bora kwenye sanaa ya 'Hope Light'


KIPI kinakera zaidi, kulipa kiingilio chako kwenye shoo ya mastaa wa Bongo Fleva kisha ukamshuhudie msanii unaemkubali akifanya shoo kwa kufuatisha CD 'play back' au kununua CD ya filamu ya staa wako umpendaye halafu ukakutana na ushubwadu?

Inakera kuona bado wale mastaa wenye majina makubwa kwenye soko la filamu wakiendelea kuachia aina zile zile za filamu kwa miaka yote, inakera zaidi kuona mastaa wakubwa wakija na filamu kubwa zenye ubora hafifu.

Nani anasema Kanumba aliondoka na movie' zake? Ni vema tukakubaliana kuwa kujiweka kando kwa wasambazaji maarufu wa filamu nchini, Steps Entertainment ndio kumechangia kushusha soko la sanaa hii ambayo ilianza kushika hatamu na kugawa ajira kubwa kwa vijana.

Pengine muda utatuambia, lakini laiti kama Steps wataamua kurudi kuwekeza kwenye filamu tena ni wazi tutashuhudia aina ya sanaa ambayo ilikosekana kwa kipindi kirefu, ni kama  ambavyo naamini kuna vijana watayafumbua macho ya wapenda maigizo kwa ubora wa kazi zao. 'HOPE LIGHT'

Nilianza kuwaona kwenye filamu ya Mimba Mbili wakimpa shavu mario Niva, nikahisi pengine wamebahatisha kwa kumpa pande Niva ambaye ni mmoja wa mastaa Bongo, nikashtushwa zaidi na kazi yao nyingine ya kitamaduni, Sufiani kabla ya kuja kuzima 'fegi' yangu kwenye mkwaju wa Kaburi Langu ambayo ndio imenifanya niogope aina ya sanaa waliyonayo hawa vijana.

Filamu bora siyo ile tu inayoakisi maisha ya jamii inayotuzunguka, kubwa ni kuweza kuwateka watazamaji wakaishi au wakatamani sanaa iliyofanyika kwenye movie yako.

Kama filamu inahusu mapenzi basi watazamaji wawehukwe na mapenzi yaliyochezwa humo, ni kama nilivyoicheki filamu ya Kaburi Yangu iliyochezwa na vijana wa Hope Light, Ally Njenje, Ayoub Taffy, Mazila na wakali wengine, sanaa imeufanya uchawi uliochezwa humo kugeuka kuwa kama kweli.

Nsyuka, Safari na Shumileta zinabaki kuwa muvi bora za kichawi zilizotoka mwanzoni lakini katika zama hizi wapenzi wa filamu watakubaliana na mimi kwamba unapoongelea filamu za kitamaduni ni Hope Light ambao wanaweza kukupa kile ambacho hutoona unadanganywa.

" Brother hii Kaburi Langu haikua rahisi, kuna scene ambayo watu walitakiwa kuzikwa kweli, yaani waingie ndani ya Jeneza halafu wafukiwe, unaweza kudhani masihara lakini tuliwafukia watu kwenye kaburi.

" Hatukutaka kufanya editing, tungeweza kufanya effect lakini kiu ya Hope Light ni kumfanya mtazamaji aone anatazama kitu halisi na siyo filamu, tulifukia wenzetu kama ambavyo mwandishi wa script alitaka," anazungumza katika hali ya kujiamini Muongozaji wa Kaburi Langu, Ally Njenje huku akinionesha vipande vya video wakiwafukia wenzao.

Mkali aliyecheza kama 'main character' na mwandishi wa filamu hiyo, Ayoub Taffy Batchu ananiongezea hii, " Mwanzoni ilitupa shida sana baada ya Kaburi Langu kutoka, watu wengi mtaani na mashabiki kwa ujumla hawakua wakiamini kwamba ile ni sanaa walidhani ni kweli nilikufa na kuzikwa.

" Muitikio wa mashabiki haukua mkubwa sana lakini hiyo bado haijatukatisha tamaa tunajua soko linataka nini, tunaamini ipo siku tutaeleweka tu mawe tuliyonayo siyo ya kawaida, ipo siku lock zitaachia tu," ananiambia huku akionesha baadhi ya script za muvi zao ambazo bado hazijatoka.

Kaburi langu ukiitazama unaiona sanaa halisi hakuna ujanja ujanja uliotumika, mazingira, wasanii wanaendana na kile kilichofanyika kwenye filamu hiyo, kiwango cha bajeti kilichotumika hakijaniridhisha kulingana na aina ya ubora uliooneshwa humo. Hata malipo waliyoyapata hayaendani na ubora wao, Kuna sehemu mashabiki tumewadhulumu hawa jamaa.

Ghafla nawaza mwenyewe ni ukubwa kiasi gani hawa mabwana wangeupata kama wangekutana na moto wa Steps, nawaza jinsi ambavyo filamu yao ingegombaniwa kwenye vibanda vyetu vya kukodisha CD uswahilini.


Ni aina ya wasanii ambao wakikupa filamu yao uiangalie wala haitokua suala la lazima kuwapa 'comment' maana wanaamini ubora wao sio wa kusubiria comment za mashabiki, hawabahatishi wana uhakika wa kile ambacho wanakitoa.

Kalamu yangu imempa Njenje ushindi katika kuandaa filamu za kitamaduni, ni kama ambavyo akili yangu inaniambia huyu Ayoub Taffy Batchu ni ushindi mkubwa wa Bongo Movie kama hatutoacha kupeana kazi kwa kuangalia majina.

Mazila aliyevuruga kwenye Mimba Mbili na Kaburi Langu ni Diva mwingine ambaye kama wadau wa filamu na watanzania tunapaswa kumpokea kwenye game ma kumuonesha kiti chake.

Wakati huu ambao naendelea kusoma miswada yao ya filamu zaidi ya 15 ambazo bado hazijatoka wacha nizime fegi yangu na kukiri wazi kwamba kama Taifa tumekuwa tukipoteza vipaji vingi kwa kugoma kuwapa nafasi wenye uwezo kwa kukumbatia wale tunaoamini ni mastaa.

Akili yangu inaniambia Hope Light ni kizazi kingine cha maajabu kwenye filamu kama tutaamua kuwapa nafasi. Ni uamuzi wetu wenyewe kuamua kutazama vilivyo vya kawaida na kuviacha vilivyo bora msituni, au kugawa nafasi kwa usawa. Ni uamuzi wangu na wako siyo Sheria.

0683 015145

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.