Zitto Kabwe asema lawama ambazo inalikumba zao la Korosho ni za Serikali
Picha ya mtandao
Kiongozi wa chama cha ACT-wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa lawama zote ambazo inalikumba zao la korosho mwaka huu ni za serikali na sio mtu mwingine yeyote.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Dar es salaam, Zitto amesema kuwa kitendo cha serikali kupitisha sheria mpya ya kuchukua pesa yote ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje ya zao hilo (Export Levy) zaidi ya shilingi bilioni 200 kutoka kwa wakulima ndiyo iliyopelekea kuyumba kwa uzalishaji.
"Sisi tulionya kuwa maamuzi hayo ya serikali yangeshusha uzalishaji, kuanzia mwaka 2012 ambapo tulizalisha tani 131,000, uzalishaji umekuwa unapanda hadi 331,000 mwaka uliopita, lakini mwaka huu makadirio ya uzalishaji yataporomoka kwa asilimia 40", amesema.
"Kwa taarifa tulizonazo kutoka kwa Bodi ya Korosho na kutoka kwa wanunuzi, mwaka huu tutavuna korosho chini ya kiwango cha uzalishaji cha mwaka 2012 ambacho ni tani 131,000", ameongeza.
"Katika hali ya kawaida ilitakiwa serikali ilichukulie zao la korosho kama zao la kimkakati, pesa yote asilimia 100 irudi kwenye korosho kwasababu ni zao la kwanza katika historia kutuingizia mapato ya dola bilioni moja, lakini serikali hii haisikii, haina maarifa ya kiuchumi na inapelekeshwa na tamaa"
Aidha kiongozi huyo ameiomba serikali inunue korosho zote za wakulima za mwaka huu kwa bei ya mwaka uliopita ili wananchi wasipate hasara, pamaoja na kuanzisha mfuko maalumu kwa wakulima wa zao hilo ' fao la bei' ili panapotokea kuporomoka kwa bei, mfuko huo uweze kuwasaidia wakulima.
No comments
Post a Comment