LUGOLA AAGIZA KUTENGULIWA VIGOGO POLISI MAUAJI YA NGURUKA UVINZA KIGOMA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP),Simon Sirro, kuwaondoa katika madaraka Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma , Mkuu wa Operesheni wa Mkoa huo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Uvinza na Mkuu wa Intelijensia wa wilaya hiyo.
Pia, Lugola ameagiza askari wote wa kituo cha polisi Mpeta na Nguruka wilayani Uvinza wahamishwe haraka iwezekanavyo katika vituo hivyo.
Lugola alitoa maagizo hayo kutokana na upungufu aliouona katika operesheni iliyofanyika mwezi uliopita ya kuwaondoa wakulima na wafugaji waliovamia enao la kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambao iko chini ya Wizara ya Mifugo, ambayo katika operesheni hiyo askari polisi wawili na raia wawili waliuawa.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kitongoji cha Mwanduhubandu, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, jana Waziri Lugola alisema viongozi hao wa polisi wameshindwa kuifanya kazi hiyo kwa umakini ndio maana kulikuwa na upungufu mkubwa katika operesheni hiyo, hivyo damu za waliouawa zinakuwa juu ya viongozi hao wa polisi mkoa na wilaya.
“Kutokana na hali hiyo, namwagiza IGP Sirro kuwaondoa kwenye madaraka hao wote niliowataja ifikapo kesho na kesho (leo),” alisema na kuongeza
“Nitakapokuwa Dodoma nitakutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ili kuona hatua nyingine za kinidhamu zitakazochukulia kwa hao niliowataja.”
Waziri Lugola aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi halina nia ya kuua mtu, kumuonea mtu, kudhulumu mtu, lakini pale inapotokea jeshi hilo limeshindwa kutekeleza wajibu wake vizuri, lazima yeye waziri achukue hatua.
Hata hivyo, Lugola alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuvunjika moyo, litaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika kuhakikisha linapambana na uhalifu, kwa hayo ambayo yanayojitokeza hayana nafasi kuwakatisha tamaa wala kuwavunja moyo.
“Mimi Waziri wa Wizara hii, dhamana yangu na haya ninayoyafanya, vyombo vyangu vya ulinzi na usalama ninavyovisimamia msinione mimi kama mwanasiasa, msichukulie maagizo yangu na matamko yangu kama ya mwanasiasa, atakayejidanganya itakula kwake,” alisema Lugola.
Wanaotakiwa kuondolewa madaraka kwa mujibu wa Waziri Lugola, ni Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wakati operesheni hiyo ilipotokea, ACP Simon Ngowi, Mkuu wa Operesheni wa Mkoa huo, SP Msembele, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Uvinza, SSP Mwakisambwe na Mkuu wa Intelijensia wa wilaya hiyo, Inspekta Dotto Daudi
No comments
Post a Comment