Cheka na Dullah Mbabe watunishiana studio
Francis Cheka (kushoto) na Dullah Mbabe (kulia)
Mabondia Francis Cheka na Abdallah Pazi maarufu 'Dullah Mbabe' wameendelea kutishiana ubabe kuelekea pambano lao kubwa litakalofanyika siku ya kufungua zawadi 'Boxing Day'.
Pambano hilo linatarajia kufanyika katika ukumbi wa Sabasaba PTA Jijini Dar es salaam.
Dullah Mbabe mwenye umri wa miaka 24, amecheza michezo 28 mpaka sasa, akiwa ameshinda mapambano 22 ambapo 21 kati ya hayo ni kwa KO, akipoteza mapambano matano na kutoa sare pambano moja.
Akizungumza katika Friday Night Live (FNL) ya EATV kuelekea pambano hilo, Dullah Mbabe amesema siri kubwa ya kushinda kwa KO katika mapambano yake ni kutokana na kuwa na nguvu nyingi kama mdudu.
"Mimi nina nguvu kama mdudu, yaani kwamba ukigombana na mimi ni sawa umegombana na kifaru, sijamuona wa kunipiga bado hapa nchini, labda mwaka 2025 nitakapokuwa mzee ndiyo labda nitapigwa," amesema Dullah Mbabe.
Kwa upande wa Francis Cheka ambaye ana miaka 36, amecheza michezo 44, ambapo ameshinda 32, akipoteza mapambano 10 na kutoa sare mapambano mawili, amesema, "ninaamini kumpiga Dullah Mbabe ni suala la kawaida kwasababu nimeshakwepa mishale mingi mpaka sasa, kila mtu atakayekuja pale ulingoni ataona, wala siongei sana".
"Ni kweli huwezi kuwa bingwa milele, hilo linafahamika kuwa watu huwa wanapokezana kwa muda. Lakini kwa sasa hivi mimi ndiyo namba moja, nimeshinda ubingwa wa Dunia mara 5, bingwa wa Afrika mara 4 na bingwa wa mabara mara 2 na sasahivi ninachofanya ni kuhamasisha vijana wanaokua," ameongeza Cheka.
Viingilio vya pambano hilo ni Sh 7,000 kwa mzunguko na Sh 15,000 kwa VIP.
No comments
Post a Comment