Followers

Namna ya kukuza na kutanua biashara yako


Toleo hili ni mahususi kwako wewe kama, ni mfanyabiashara ndogondogo, au ni mfanyabiashara mkubwa na ungependa kukua zaidi, au kama wewe una nia ya dhati ya kuanzisha na kuendeleza biashara yoyote inayokidhi misingi ya haki na sheria za nchi.

Karibu. Kama mfanyabiashara siku zote unatizama katika upande bora zaidi, upande wa maendeleo. Hii ina maana siku zote unapenda kuiona biashara yako ikikua na kupanuka zaidi, unaweza kuwahudumia wateja wengi zaidi na faida inazidi kuongezeka.

Haya ni mambo 5 ya msingi kama una nia ya kukuza biashara yako hasa katika nchi za Afrika Mashariki. Ni muhimu kutambua kwamba jirani yako kabisa Mama Jofre au yule msukukuma guta anayetumia bidhaa zako ndiye atakayekukuza wewe. Biashara huanza kutanuka kuanzia chini kabisa nikimaanisha kwamba mteja aliye karibu na biashara yako ndiye anayeweza kusema mema kuhusu biashara yako akaaminika zaidi kuliko tangazo lako lililogharimu zaidi ya milioni mbili kuruka hewani.

1. Katika biashara hasa ndogondogo ni muhimu kufahamu soko lako liko wapi na kama bidhaa yako inaweza kujiuza. Utakapogundua ni wapi soko lako lilipo anzia hapo, ongeza juhudi, ubunifu na ustadi wa huduma. Kwa mfano muuza senene kutoka Kagera unapogundua kwamba watu waishio Dar es Salaam ndio hununua zaidi biashara yako, wapelekee huduma, jenga mabanda Dar es salaam
au ongeza idadi ya vijana wanaotembeza biashara yako. Fuatilia ni aina gani ya senene wanaopendwa zaidi, Je, ni wale wenye pilipili au wenye iriki au wale wenye pilipili na iriki pamoja. Fuatilia je, ni wale waliokauka sana au kiasi. Ukishagudua ni wapi wanaouza zaidi, ongeza mzigo wako. Watengeneze kama soko lako linavyowahitaji kisha ingiza sokoni, utauza na ukiuza utapata pesa zaidi.

2. Jambo la pili ni jinsi ya kutumia pesa baada ya kupata pesa zaidi.Wengi huadaika na kuwa na pesa nyingi katika wallet, M-PESA, Airtel Money au Tigo Pesa zao. Usiende baa kuwazungushia marafiki zako raundi kisa pesa imepatikana nyingi zaidi ya ile uliyoitarajia. Simaanishi kwamba usifurahi na wenzako au ujitenge na rafiki zako, La Hasha! Fanya kwa kiasi kidogo sana. Kwa nini ninasema kiasi kidogo sana? Bila shaka wewe bado ni mdogo sana katika biashara. Hivyo unahitaji kila senti unayoweza kuitengeneza katika kukuza biashara yako. Usipende starehe sana. Usipende kutumia pesa ili kuonesha kwamba una pesa. Badala yake wekeza pesa hiyo katika bishara yako hiyohiyo na utaona jinsi pesa iatakavyozidi kuongezeka. Kama unauza chipsi, gunia moja limemalizika na umefanikiwa kupata pesa zaidi usitake kununua gunia moja tena. Jiwekee deni sasa ununue magunia mawili. Yakimalizika pesa itakua nyingi zaidi, usitatake kununua magunia mawili tena jiwekee malengo ya kununua magunia matatu. Kwa jinsi hii biashara yako itaanza kukua, utapata wateja zaidi.

3. Jambo la tatu ni kuwa mkweli na muwazi. Siku zote msema uongo ni mpenzi wa shetani, na wapenzi wa shetani, wow! hawafanikiwi na ni wabaya. Usipende kutoa sababu zisizo za msingi katika biashara yako. Kwa mfano, kama una biashara ya mama n'tilie usiwalishe wateja mchuzi uliobaki jana na kisha wakilalamika ukasema kwamba tatizo limetokea katika bucha ya nyama.

Lakini zaidi lipa kodi kama bishara yako inahitajika kulipia kodi. Ukiwa muwazi kwa mamlaka ya kodi huweza kukusikiliza na kukusamehe kodi kiroho safi tu hasa kama biashara yako ni ndogo. Lakini ukianza kuleta uongo, mara ukiwaona TRA unafunga duka, au unajificha kabatini ukisikia hodi ya mama mwenye pango biashara yako itayumba na hautaweza kupanuka. Isajili biashara yako na hii itakusaidia sana mbeleni.

4. Jambo la nne ni kujitanua kwa kukuza network, kujuana na watu, kuungana na bishara nyingine katika kutoa huduma zako. Jaribu kuwafanya watu wengi zaidi wakufahamu. Ziko njia nyingi sana za kufanya hivi lakini moja ni kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabisahara wenzako. Kama Bwana Juma na Bwana Zengwe ni wafanyabishara wenye mahusiano mazuri lakini wanamiliki biashara tofauti, mteja akienda kwa Bwana Juma kuulizia huduma au bidhaa fulani akakosa, ni rahisi kwa Bwana Juma kumuelekeza mteja huyo moja kwa moja hadi kwa rafiki yake Bwana Zengwe ambaye yuko na bidhaa au huduma hiyo. Hivyo ni muhimu sana kukuza mtandao wako katika kila wilaya angalau ujulikane hii itakuwia rahisi hata kutanua wigo wa soko lako. Lakini pia kama wewe unauza mabati ni vizuri ukaungana na mfanyabiashara anayeuza cement na pamoja mnaweza kuunda biashara ya mabati na cement hivyo kuwavutia wateja wengi zaidi.

5. Jambo la tano ni kujaribu kuteka biashara nyingine na kufanya juhudi ya kupata tenda za serikali. Hauwezi kushinda tenda za serikali kama haujasajili biashara yako. Lakini hakika kama utaweza kupata tenda za serikali basi biashara yako itapanuka kwani tenda hizi huhitaji bidhaa nyingi sana hivyo pesa nyingi pia lakini serikali ni mteja mzuri sana. Kama umeweza kufanya biashara na serikali hata ya kuwauzia kuni tu, utashindwa kufanya biashara na nani? Jambo jingine ni kujaribu kuanzisha biashara nyingine. Kwa mfano kama umeanza na biashara ya kubrashi viatu, sio vibaya unapokuza mtaji wa viatu ukaanzisha biashara nyingine ya kuuza malapa, viatu, mikanda au soksi. Hii itakupa mwanya wa kutegemea zaidi ya biashara moja katika kujipatia mapato yako. Hivyo itakuza biashara yako.

Kama unavyofahamu biashara inahusisha kujaribu na kuwa tayari kwa hasara na faida. Lakini biashara sio mchezo wa bahati nasibu kwamba ukipata umepata, ukikosa umekosa. Hata ukipata ni muhimu kujidhatiti zaidi ili uzidi kukua na kama ukikosa hata siku moja usije kukata tamaa. Endelea kupambana na kama ukifuata njia sahihi za kutoa huduma hata siku moja hautashindwa lazima iko siku biashara itajibu na utaendelea kupanuka zaidi. Watu wote waliofanikiwa wamewahi kupitia vipindi vigumu, kampuni ya vifaa vya elektroniki ya Apple, iliwahi kufikia hatua ya kuuza baadhi ya haki na viwanda vyake ili iepuke kufirisika kabisa. Apple iliamua kubadili uongozi wake na kupunguza kazi wafanyakazi wengi sana, lakini kwa kichache Apple ilichobakia nacho chini ya mfanyabiashara wa kuigwa Steve Jobs, waliweza kuanza upya na mpaka sasa mafanikio yake wote yunajionea.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.