Followers

RPC: Mbwa kuongoza Doria Krismas na Mwaka Mpya, Ulinzi kuimarishwa.



Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa limedhamiria kuimarisha ulinzi zaidi katika kipindi hiki cha Sikukuu za Krismas na mwaka mpya ili wakazi wa mkoa huu waweze kusherehekea bila bughudha ya aina yoyote.

Akitoa salamu za heri ya Sikukuu ya Krismas na mwaka Mpya kwa wananchi wa mkoa huu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ramadhani Ng’anzi amesema kwamba wamejipanga vizuri kuhakikisha kwamba usalama unazidi kutawala zaidi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu.

“Kama tunavyofahamu mkoa huu umekuwa  ni miongoni mwa mikoa yenye utulivu wa hali ya juu hapa nchini na wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi bila shaka lakini tumeamua kuongeza ulinzi zaidi hasa kwa kutumia Mbwa wetu ambao watakuwa kila kona katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha doria”. Alisema Kamanda Ng’anzi.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba ili kuhakikisha utulivu huo unadumu kwa kipindi chote, kwa mwezi huu wa Disemba na kuendelea wamefanya misako kabambe ambayo imefanikisha kupatikana kwa vifaa mbalimbali pamoja na watuhumiwa.

Katika misako hiyo Jeshi hilo lilifanikiwa kuwapata watuhumiwa (Majina yanahifadhiwa) wakiwa na vifaa vya kuvunjia ambao wanashiriki katika matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo Wizi ndani ya gari, ambapo walikutwa na Lap Top Nne, I Pad mbili, Flat Screen, simu Tisa (Smart Phone) pamoja na pikipiki mbili pamoja na vifaa mbalimbali huku akiwataka waliobiwa waje katika kituo kikuu cha Polisi Arusha na kutambua mali zao.

Aidha Kamanda Ng’anzi amewataka wakazi wa mkoa huu kutotoa mwanya kwa wahalifu kwa kuacha nyumba zao bila kuwa na muangalizi pindi wanapotoka lakini pia amewaasa wazazi kuwa waangalifu kwa watoto wao wenye umri mdogo pindi wanapotembea nao barabarani na kupiga marufuku Disco Toto katika kumbi mbalimbali za Starehe.

Akizungumzia shamrashamra za kuukaribisha mwaka wa 2019 Kamanda Ng’anzi amewaonya watu watakaothubutu kufanya fujo kama vile kuchoma matairi barabarani, kuendesha vyombo vya moto kwa bila kuzinagatia sheria za usalama barabarani na hata kufyatua Fataki bila kibali watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kamanda Ng’anzi amewatakia wananchi wote wa mkoa huu Heri ya Sikukuu ya Krismas na mwaka Mpya wa 2019 na kuwashukuru kwa ushirikiano wao walioutoa kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu hali ambayo inasaidia kuimarisha usalama na kuwasihi waendelee kuwa pamoja na Jeshi hilo.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.