Wachezaji Yanga SC wawatoa hofu mashabiki
Mastaa wa timu ya Yanga SC wamefunguka baada ya timu hiyo kupokea vichapo mfululizo na kuwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kutamba kuwa bado lengo lao ni kuhakikisha wanatwaa makombe mawili msimu huu.
Kauli hiyo wameitoa ikiwa ni siku chache tangu watoke kufungwa mchezo wa ligi na Stand United kwa bao 1-0 na ule wa robo fainali ya SportPesa Cup dhidi ya Kariobangi ya nchini Kenya kwa mabao 3-2.
Timu hiyo itaingia tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Alhamisi ijayo katika mchezo wa FA watakapovaana na Biashara FC ya Mara.
Nyota Juma Abdul, Mrisho Ngassa na Amissi Tambwe walisema wao kama wachezaji wamekuwa wakijadiliana mambo kadhaa ya kuhakikisha timu yao inapata ushindi na kuchukua ubingwa wa ligi kuu kama walivyopanga.
Tambwe alisema kupoteza mchezo mmoja kwenye ligi siyo sababu ya wao kupoteza ubingwa wa ligi zaidi watajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo ijayo.
“Kiukweli malengo yetu ni kutwaa ubingwa, hakuna mchezaji ambaye hatambui hilo na ndiyo sababu ya kila mechi kwetu huwa tunacheza kama fainali kwa kuwa tunahitaji matokeo, maana bado kuna mechi nyingi na wapinzani wetu wamekuwa wakifukuzia kutokana na ushindani ulivyo.
Mpaka sasa kwenye ligi, Yanga imecheza mechi 20 imefanikiwa kushinda mechi 17, ikitoka sare mbili huku ikipoteza mchezo mmoja hali inayompa matumaini mshambuliaji huyo mwenye mabao sita msimu huu kuweza kutwaa ubingwa.
No comments
Post a Comment