Followers

Weusi wawajibu wasanii wa Kenya kampeni ya ‘Play Kenyan Music’


Weusi wawajibu wasanii wa Kenya kampeni ya ‘Play Kenyan Music’

Kundi la muziki wa rap na hip-hop la ‘Weusi’ linaloundwa na wasanii watano kutoka Arusha, limewajibu wasanii wa Kenya wanaoendesha kampeni inayotaka vyombo vya habari nchini humo kucheza muziki wa ndani na kuachana na muziki wa nje ya nchi.

Wakifunguka mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia XXL ya Clouds FM, wasanii wa kundi hilo ambalo linatajwa kuwa kundi bora la hip-hop lililodumu katika kipindi cha hivi karibuni, wamewataka wasanii wa Kenya kukubaliana na soko huria la muziki na kujikita katika kutengeneza ngoma kali zitakazopenya kwenye soko la ushindani.

Weusi wamewakumbusha wasanii wa Kenya kuwa kuna wakati fulani nyimbo zao zilifanikiwa kuteka soko hadi la Tanzania na kuwafanya wasanii wa Tanzania kuumiza vichwa zaidi.

“Mbona enzi zile akina Jua Kali, Nonini, Nyota Ndogo walikuwa wanapiga mashow Tanzania… hatukuwa na noma. Hadi tamthilia ya Tausi ilikimbiza Bongo lakini haikuwa noma yoyote,” alisema Nikki wa Pili.

Wakitumia utani wa lafudhi ya Nairobi (sheng’), wasanii hao waliwataka Wakenya kutulia kidogo ili na wao watengeneze ‘chapaa kiasi’ kama ilivyokuwa enzi zile Wakenya walivyotengeneza ‘chapaa’ kutoka Tanzania.

Nikki wa Pili alitoa hoja kuwa kosa la kiufundi lililofanywa nchini Kenya ni kuweka sheria ya vyombo vya habari kuwalipa wasanii kwa kucheza nyimbo zao lakini sheria hiyo haikuhusisha nyimbo za nje ya nchi.

“Nadhani kitu ambacho walijichanganya pia ni kuweka malipo ya mirabaha kwenye nyimbo za Kenya zinapochezwa na vituo vya ndani halafu wakaacha nyimbo za nje. Kwa kawaida mfanyabiashara huwa anakimbilia kwenye unafuu, kwahiyo vyombo vya ndani vikaona ni bora vicheze nyimbo za nje kwa wingi ambazo hawazilipii ili kupata unafuu wa gharama,” alisikika Nikki wa Pili.

Nikki wa Pili, Lord Eyez, Joh Makini na G Nako wameachia wimbo mpya ‘Wapoloo’ uliopikwa ndani ya studio za Switch Studio na mtayarishaji Ammy Waves. Wimbo huo umeonekana kufanya vizuri ndani ya wiki moja ya kwanza.

Wasanii wengi wa Kenya wameunga mkono kampeni ya ‘Play Kenyan Music’ (cheza muziki wa Kenya), wakipinga hatua ya vyombo vingi vya habari kucheza asilimia 30 tu ya muziki wa Kenya huku wakizipa nafasi zaidi nyimbo za Tanzania, Uganda, Nigeria na Afrika Kusini.

Katika miaka ya hivi karibuni, wasanii wengi wa Tanzania wameonekana kufanya vizuri nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kufanya matamasha makubwa nchini humo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Juma Nature, Diamond, Ali Kiba, Harmonize na wengine walifululiza kufanya matamasha makubwa nchini humo.

Ni dhahiri, kuna wasanii wachache wa Kenya wanaofanya vizuri nchini Tanzania ukilinganisha na wasanii wa Tanzania wanaofanya vizuri nchini Kenya. Bongo Fleva imeiteka Kenya kuliko ilivyo Genge kwa Tanzania

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.