Angalia Mikocheni ilivyoathiriwa na mvua
MVUA zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es salaam zimeendelea kuleta madhara katika maeneo ya Mikocheni barabara ya Chato mtaa wa Lukuledi baada ya barabara hiyo kukatika na kujaa maji.
Akizungumza na Michuzi Blog, Kaimu Meneja uhusiano wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam(DAWASCO) Everlasting Lyaro ameeleza maji hayo ni ya mvua na karavati linalomwaga maji hayo ni yale yanayokusanywa maeneo ya Mwenge, Mwananyamala na Mikocheni.
Aidha ameeleza walienda eneo la tukio na kugundua tatizo hilo halikuwa lao bali ni watu wa ujenzi wa barabara chini ya Manispaa na tayari suala hilo limekabidhiwa kwa makandarasi waliojenga barabara hiyo.
Pia ametoa rai kwa wananchi kwa kuwataka kuhifadhi miundombinu hasa mita zitakazosombwa na maji na watakaokumbwa na tatizo hilo watarekebishiwa mita hizo bure. Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa maeneo yatakayokosa huduma ili washughulikie mara moja.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo Abdul Rashid ameeleza tukio hilo lilianza jana saa nane mchana baada ya magari kadhaa kupita ghafla barabara ilishuka na maji kuanza kumwagika hali iliyosababisha barabara kushindwa kupitika na ugumu wa biashara.
Hadi waandishi wetu wanaondoka eneo la tukio sehemu ya barabara hiyo iliendelea kukatika.
No comments
Post a Comment