Askofu Banzi: Tuwaheshimu Marehemu, Tusiwafunge Kwenye Viroba
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi ameitaka jamii kuiheshimu miili ya marehemu kwa kuwapa maziko ya heshima badala ya kuwafunga kwenye viroba na kuwatupa kwenye maji.
Amesema jambo ambalo si zuri machoni kwa wanadamu na kwa Mwenyezi Mungu na pia inakiuka utamaduni wetu kama Watanzania ambapo ameitaka jamii kubadilika kwa vitendo vya namna kwani vinaondoa utu wao.
Ameyasema hayo leo Jumapili Aprili Mosi, wakati akitoa salamu za Pasaka kwa waumini wa kanisa hilo kwenye misa iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Anthony wa Padua, Chumbageni Jijini Tanga.
“Lazima tuwaheshimu marehemu katika nchi yetu, pengine tunataka kuwa na utamaduni tofauti wafu wengi tunaambiwa wameokotwa ndani ya viroba kwenye maji na kuzikwa, je hali hii inatupeleka wapi kama taifa” Tujitafakari kwa jambo hilo.
“Kama unavyoheshimika ukiwa mzima, marehemu pia wanapaswa kuheshimika hata wanapokuwa wamefariki kwa kuhifadhiwa mahali ambapo hawawezi kuonekana tena,” amesema.
Aidha, amewataka viongozi ambao wanajukumu la kulinda usalama wa nchi, kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu ambayo ni tunu tulioachiwa na waasisi wa taifa hili.
“Mara nyingi tumesikia raia wema wametoa taarifa ya kukamatwa wahalifu hivyo ni jukumu la waliochaguliwa kutazama usalama wao kwa lengo la kuwawezesha kutimiza majukumu mengine ya kimaendeleo,” amesema Askofu Banzi.
No comments
Post a Comment