Followers

Fanya haya uepukane na vijiwe kwenye figo


Kama una imani haba unaweza kukubaliana na wenye imani potofu au za kishirikina kuwa umefanyiwa hayo mambo pale daktari anayekuhudumia atakapokujulisha kuwa una vijiwe kwenye figo.

Tatizo la kuwa na vijiwe katika figo na mfumo wa mkojo(kibofu cha mkojo) kwa ujumla

Mawe haya hutokana na madini chumvi au tindikali mbalimbali zinazotolewa mwilini.

Zipo aina tatu za mawe hayo ikiwamo vijiwe vya calcium oxalate, vijiwe vya tindikali ya uric (uric acid), vijiwe vya struvite (magnesium, ammonium na phosphate).

Mawe haya huwa na maumbile tofauti, yanaweza kuwa madogo kuliko changarawe au kubwa kuliko yai au mpira wa tenisi. Yanaweza kuwa na nyuso laini kiasi chakutoleta maumivu au kuwa na nyuso zenye manundu nundu.

Swali kubwa wanalojiuliza watu wengi je mawe haya yanatoka wapi?

Kisayansi mawe haya husababishwa na kukosekana kwa usawa wa maji, madini (chumvichumvi) na tindikali za mwilini, jambo hili kitabibu hujulikana kama electrolyte imbalance. Vitu hivi tunavipata kwakula vyakula mbalimbali na baadhi ya dawa.

Yapo maradhi mbalimbali yanayohusishwa na kutokea kwa mawe hayo mwilini ambayo husababisha ugonjwa wa utindikali kwenye mirija ya figo.

Pia, matatizo kwenye tezi za parathyroid, kukojoa chumvi chumvi za oxalate kupita kiasi na hali ya nyama za figo kuwa sponji.

Tatizo hili huwapata zaidi watu walio na historia kwenye familia yao ya kuwa na vijiwe kwenye figo, watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea, ingawa tatizo hili llinaweza pia kumpata mtu wa umri wowote.

Lakini pia jinsia ya mtu ni kigezo chakupata tatizo la kuwa na mawe kwenye figo. Ila wanaume wako katika hatari zaidi ya kupata maradhi hayo kuliko wanawake.

Watu wengine ni wale wenye upungufu wa maji mwilini hasa wenye hulka zakutopenda kunywa maji yakutosha kwa siku kama madaktari wanavyoshauri.

Vile vile, ulaji wa kiasi kikubwa cha protini, chumvi na sukari, watu wenye umri mkubwa ambao ni wanene kupita kiasi, ambao kitabibu huitwa ‘Obesity.’

Watu wenye ugonjwa wa utumbo mkubwa uitwao inflammatory bowel diseases na waliowahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo ujulikanao kama gastric bypass surgery.

Mambo haya ndiyo yanamweka mtu katika hatari yakupata tatizo hilo

Dalili ni pamoja na kuhisi maumivu makali ya tumbo hasa sehemu za mbavu. maumivu haya huwa na tabia ya kuja kwa ghafla, kudumu kwa sekunde kadhaa kisha kuachia.

Maumivu haya wakati mwingine huweza kushuka kuelekea kwenye ncha ya uume kwa wanaume na kwa wanawake huelekea kwenye kinena, kujihisi kichefuchefu na kutapika

Dalili zingine zipo zaidi katika mfumo wa mkojo ikiwamo kukojoa mkojo uliochanganyika na damu. Wakati mwingine uwapo wa usaha katika mkojo kama kuna maambukizi ya bakteria.

Pia, maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kutoka kwa kiwango kidogo sana, kupita kwa tabu katika mirija inayotoa mkojo toka katika figo kuja katika kibofu.

Hali hii husababisha figo kushindwa kutoa uchafu mwilini na kusababisha mlundikano mkubwa kwenye damu. Huwa ni sumu mbaya mwilini.

Kushindwa kupita kwa mkojo husababisha pia kutanuka kwa sehemu za figo ikiwamo ile inayoitwa kitabibu Renal pelvis na calyces, kitabibu inaitwa Hydronephrosis.

Kama kutakuwa na maambukizi katika mkojo (Urinary Track Infections-UTI) mgonjwa anaweza kuwa na homa na uchovu wa mwili.

Dalili zingine zinaweza kujitokeza kutokana na ukubwa wa madhara ya tatizo.

Vipimo vinavyoweza kugundua tatizo hilo na madhara yake ni picha ya X-ray inayoonyesha mfumo mzima wa figo, mirija ya ureta pamoja na kibofu cha mkojo.

Kipimo kingine huitwa intravenous pyelogram (IVP), vipimo vya picha za CT-scan au MRI

Vile vile, Ultrasound ya tumbo, kipimo cha mkojo na kuotesha (urine culture and sensitivity) na kipimo cha kuonyesha hali ya chembe hai za damu (FBP).

Matibabu ya vijiwe katika figo hutegemea na ukubwa wa vijiwe husika. Kama vidogo na dalili alizo nazo mgonjwa ni chache hazimzuii kuendelea na kazi zake za kila siku, mgonjwa anashauriwa kunywa maji mengi kiasi cha lita mbili hadi tatu kwa siku.

Hii husaidia kuviondoa vijiwe kutoka katika figo au njia ya mkojo. Nyingine ni kutumia dawa za maumivu alizoshauri daktari ili kupunguza maumivu yanayojitokeza.

Kama vijiwe ni vikubwa na dalili ni nyingi zinazoweza kumfanya mgonjwa ashindwe kuendelea na kazi zake za kila siku, anaweza kutibiwa kwa kutumia vifaa tiba vifuatavyo;

Mawimbi mtetemo kutoka nje ya mwili, kifaa tiba hiki huweza kuvunjavunja vijiwe na kisha hutolewa nje kupitia kwenye mkojo.

Njia nyingine ni ya upasuaji na kisha kuvitoa vijiwe hivyo (percutaneous nephrolithotomy), kwa kutumia kifaa maalumu kiitwacho ureteroscope.

Wakati mwingine upasuaji wa kuondoa tezi za Parathyroid hufanyika kama chanzo kitakuwa ni tatizo la hyperparathyroidism.

Vile upasuaji wa kisasa kwa njia ya kamera na kifaa cha upasuaji na kifuko huweza kuingizwa kwa njia ya matundu na kuviondoa vijiwe hivyo.

Namna ya kuzuia tatizo la mawe katika figo

Mambo unayoweza kufanya kuzuia tatizo la vijiwe kwenye figo ni pamoja na kuhakikisha kuwa unaepuka mambo yote hatarishi ambayo nimeyataja.

Jenga tabia ya unywaji wa maji mengi kwa siku na kuhakikisha unakojoa angalau lita 2.5 za mkojo kila siku. Mtu mzima akiweza hata lita 1.5 -2 za maji. Kumbuka hata vyakula tunavyokula vina majimaji.

Jenga tabia ya kubeba chupa ya maji na kuyanywa mara kwa mara, ukiweza kunywa glasi 12-14 kwa siku. Ili kujua umekunywa maji mengi yakutosha rangi ya mkojo haitakua njano yenye ukali.

Tumia matunda yenye maji kwa wingi ikiwamo kama juisi ya maji ya madafu, tikiti maji, nyanya na matango.

Punguza utumiaji wa vyakula vyenye oxalate kama viazi vitamu, spinach, soya, chai na chocolate. Hasa walio katika hatari watumie kwa kiasi na si kuacha kabisa.

Kula vyakula vyenye chumvi kidogo epuka tabia ya kuongezea chumvi mezani na punguza kula protini hasa itokanayo na nyama. Tumia itakonayo na jamii ya kunde na maharage.

Madini ya Potassium citrate husaidia kuongeza ukakasi (PH) hivyo kuzuia wingi wa tindikali katika mwili.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.