Kuzuia kifafa cha mimba fanya haya
Kifafa cha mimba ni ugonjwa unaohusiana na msukumu mkubwa wa damu (high blood pressure) wakati wa ujauzito pamoja na kuharibika viungo muhimu vya mwilini kama ini na figo.
Kwa kawaida, ugonjwa huu Hutokea baada ya nusu ya kipindi cha kwanza cha ujauzito kuisha (kuanzia wiki ya 20 au baada ya miezi mitano kuisha).
Ugonjwa huu unaweza kuwatokea ata wajawazito ambao hawakuwai kuwa na tatizo la msukumo wa damu kabla ya ujauzito.
Maradhi hayo husababisha matatizo makubwa kwa mjamzito na mtoto alie tumboni kiasi hata cha kuharibu viungo muhimu ikiwamo figo na ini la mjamzito na kumuweka katika hatari ya kupoteza maisha kama hatapatiwa huduma haraka. Pia, mtoto aliyeko tumboni anaweza naye kupata madhara kwa kukosa damu ya kutosha kutoka kwa mama na kushindwa kukua vizuri iwapo hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu, mtoto anaweza kufia tumboni.
Kutokana na hathari kubwa za ugonjwa huo kwa mjamzito na mtoto aliye tumboni, inashauriwa kila mjamzito ahudhurie kiliniki kusudi apimwe msukumo wa damu (blood pressure) na mkojo kwa lengo la kuhakikisha yuko salama.
Kama kipimo cha msukumo wa damu ni kikubwa kuliko 140/90mmHg, ni muhimu kurudia kipimo hicho baada ya muda pamoja na kufanya vipimo vingine vya maabara vinavyoweza kujulisha uwapo wa kifafa cha mimba.
Sababu za ugonjwa huo kutokea hazijulikani mpaka sasa ingawa zipo nadharia mbalimbali zinazojaribu kuelezea. Moja ya nadharia inasema sababu ya ugonjwa huo kutokea ni matatizo ya ukuaji wa kondo la nyuma (placenta).
Mishipa ya damu inayounda placenta ikikosea jinsi ya kujikita kwenye ukuta wa kizazi, husababisha mishipa hiyo kuwa na tabia tofauti na ile ya kawaida na kusabibisha mjamzito kupata msukumo wa damu mkubwa tofauti na wa kawaida na kupata kifafa cha mimba.
Nani aliyekatika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo?
Wanawake ambao wanashinikizo la damu, kisukari, unene kupita kiasi na wale wanaougua figo kabla ya ujauzito, wana uwezekano mkubwa wa kupata kifafa cha mimba.
Kwa sababu hii wajawazito wanashauriwa kufuatiliwa kwa karibu na mtaalamu wa afya kwa kipindi chote apaokuwa amebeba mimba.
Pia, mjamzito aliyepatwa na kifafa cha mimba awali kabla ya kushika ujauzito mwingine, ana uwezekano mkubwa wa kuugua tena. Wataalamu wa afya wamegundua kuwa mwanamke anayezaa na mwanaume mwingine tofauti na aliyezaa naye awali, hatari ya kuugua kifafa cha mimba ni kubwa.
Mjamzito mwenye miaka zaidi ya 40 yuko katika hatari kubwa ya kuugua kifafa cha mimba.
Hizi ndiyo dalili za kifafa cha mimba
Kwa kawaida ugonjwa huu mjamzito anakuwa nao kwa muda fulani bila kujijua wala kuona dalili zozote.
Lakini ghafla mjamzito anaweza kuona dalili ikiwamo ya kuugua tumbo juu ya kitovu, kutapika, macho kutokuona vizuri, kuumwa kichwa, mkojo kuwa na rangi isiyo ya kawaida, kupumua kwa shida, uchovu na maumivu ya viungo au kupoteza fahamu na kupatwa na degedege.
Inashauriwa kila mjamzito aonapo dalili hizo, vyema akawahi hospitali kusudi apate vipimo na matibabu au ushauri wa nini afanye.
Ingawa hakuna kinga ya uhakika ya kifafa cha mimba, wanawake walio kwenye makundi yaliotajwa hapo juu, wanao uwezekano mkubwa wa kupata kifafa cha mimba lakini wanaweza kujikinga kwa kutumia vidonge vya aspirini na calcium. Kabla ya kuvitumia vidonge hivyo, ni vyema ukapata ushauri wa kitaalamu.
Tiba pekee ya kifafa cha mimba ni kumzalisha mjamzito, hii ni kwa sababu ugonjwa huu unasababishwa na kuwapo kondo la nyuma ndani ya kifuko cha uzazi. Bila kulitoa, mjamzito hawezi kupona. Iwapo ugonjwa huo utagundulika kabla mtoto hajakomaa na kuwa tayari kwa kuzaliwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa alazwe na kuangaliwa kwa karibu wakati ikisubiriwa kukomaa kwa mtoto. Vilevile, daktari anaweza kushauri mjamzito apewe dawa ya kuharakisha kukomaa kwa mapafu ya mtoto.
Kama hali ya mjamzito itazidi kuwa mbaya, madaktari watalazimika kumzalisha hata kama mtoto hajakomaa, kwa sababu akiachwa atakuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha au mtoto kufia tumboni.
Pia, hali hiyo ikiachwa inaweza kumfanya mjamzito kupatwa na degedege, kupoteza fahamu sambamba na kupoteza uwezo wa damu na kumfanya apoteze damu nyingi wakati wa kujifungua na kuziba mishipa.
Kwa maoni na ushauri wasiliana na Dk ravinder 0746002537
No comments
Post a Comment