Followers

Manara: Sisi kama timu tumejipanga vizuri kuelekea mchezo huo




Afisa habari wa Klabu ya vinara wa ligi kuu Tanzania Bara Simba, Haji Manara amesema watajitahidi kufanya kila wawezalo ili mradi watoke na ushindi wa alama tatu katika mechi yao dhidi ya Yanga japokuwa wanatambua timu hiyo kuwa nzuri na kongwe kama walivyo wao.

Manara amebainisha hayo leo Aprili 27, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za klabu hiyo zilizopo Kariakoo eneo la Msimbazi Jijini Dar es Salaam.

"Sisi kama timu tumejipanga vizuri kuelekea mchezo huo na kikosi chetu kimesharejea Jijini Dar es Salaam jana jioni kikiwa kinatokea Mkoani Morogoro. Hali ya wachezaji iko vizuri na wapo vitani kwa sasa nikiwa na maana wapo tayari kwa mpambano. Tunajua tunaenda kupambana na timu nzuri, Yanga sio timu ya kuibeza kwa sababu wanashika nafasi ya pili wakiwa nyuma yetu na ndio mabingwa watetezi kwa hiyo tunawaheshimu kama timu kongwe tulivyo sisi lakini tunachokitafuta ni alama tatu", amesema Manara.

Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "tunahitaji alama tatu katika mechi yetu ambazo tukifanikiwa kuzipata Inshallah zitakuwa zimetuweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuchukua ubingwa".

Simba na Yanga watashuka dimbani Aprili 29, 2018 katika dimba la Taifa Jijini Dar es Salaam mchezo utakaopigwa majira ya saa 10:00 kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.