Mfu Aliyerudiwa na Uhai -01
Naitwa Esma Mabruki, lakini watu wangu wa karibu walinikatisha na kuniita Esy. Mpaka leo Esy ndilo limekuwa maarufu.
Ni mzaliwa wa Dar es Salaam. Nilizaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala na wazazi wangu walikuwa wakiishi hapohapo Mwananyamala.
Baba yangu mzee Mabruki alikuwa akifanya kazi ya udereva kwa mfanyabiashara aliyeitwa Saidi Omar au Alhakim. Kulikuwa na siku ambapo lilitokea tukio lililosababisha mguu wa baba yangu usagwe baada ya gari la polisi kuligonga gari la baba wakati likifukuza gari lililodaiwa kuwa na magaidi.
Baba alilazwa hospitali kwa miaka miwili. Madaktari waliuunga mguu wake kwa vyuma na akafanikiwa kuwa na miguu yake miwili. Baba aliporudi nyumbani, Alhakim alikuwa anafika kumsalimia. Hapo nyumbani ndipo Alhakim aliponiona na kunifahamu.
Siku nyingine nilikutana naye wakati ninatoka shule akasimamisha gari lake na kunipa lifti.
Alikuwa mtu mnene aliyekaribia umri wa miaka sitini. Alikuwa na nywele nyeupe anazoziziba kwa kofia yake ya darizi. Akaniuliza nilikuwa ninasoma kidato cha ngapi. Nikamwambia ninasoma kidato cha tatu.
“Mwakani ndiyo namaliza kidato cha nne.”
“Mmezaliwa wangapi?”
“Watano, lakini mwanamke ni mimi peke yangu.”
“Wewe ni wangapi?”
“Mimi ni wa mwisho.”
Tulipokuwa tunakaribia kufika nyumbani, Alhakim alitoa shilingi laki mbili akanipa kasha akasimamisha gari.
“Nadhani kwa hapa unaweza kwenda mwenyewe. Kuna mahali ninataka kufika. Naona nikuache hapa.”
“Asante, ninashukuru.”
Nikafungua mlango wa gari na kushuka kisha nikaanza kutembea kwa miguu. Baada ya kupiga hatua kumi hivi, niligeuka nyuma kumtazama. Niikaona hakuondoka. Alikuwa ameduwaa, akinitazama kwa nyuma. Alipoona nimemuona akaliondoa gari haraka na kwenda zake.
Nikaendelea na safari yangu hadi nyumbani. Sikuweza kufahamu kwa nini yule mzee amenitazama vile na alipoona nimemuona, akaliondoa gari haraka. Kwa vile nilikuwa ninazifahamu tabia za baadhi ya wanaume sikuendelea kumfikiria nikaendelea na shughuli zangu.
Siku iliyofuata ilikuwa ni sikukuu, hakukuwa na masomo. Alhakim na mwenzake ambaye sikumfahamu walifika nyumbani kumsalimia baba. Walizungumza chumbani mwake kwa karibu saa nzima kisha wakatoka. Ilipofika usiku wakati nimekaa na mama sebuleni akaniambia.
“Mwanangu umepata mchumba…”
Nikashtuka na kumuuliza.
“Ni nani?”
“Saidi Omar (Alhakim).”
Nikaduwaa kidogo. Nilifikiria alivyonipa zile laki mbili za bure nikafikiria vile alivyokuwa amesita, akinitazama wakati aliponishusha baada ya kunipa lifti. Kumbe kunitazama kule alikuwa na lake.
“Sasa yule si kama baba yangu?” Nikamuuliza mama.
“Kama baba yako kivipi?”
“Ni mtu mzima kisha yuko na baba.”
“Utu uzima wake si tatizo. Mwanaume hana cha utu uzima. Mwanaume mzee anaweza kumuoa binti mdogo. Lakini yule tumempenda kwa sababu ni mtu mwenye uwezo wake.”
“Kwani hana mke.”
“Amesema aliachana na mke wake.”
“Ana watoto.”
“Umeshasema ni mtu mzima, atakosa kuwa na watoto?
Watoto anao!”
“Kwa hiyo baba amemkubali?”
“Amempa sharti lake, amemwambia atoe kifunga uchumba cha shilingi milioni mbili, amekubali.”
“Sasa mama si mnafahamu kuwa ninasoma. Atanioa vipi?”
“Atakusubiri umalize masomo yako ndiyo akuoe.”
Kilichonifanya nisite sana ingawa Saidi Omar au Alhakim alikuwa na uwezo wa kipesa ni kwamba nilikuwa na mpenzi wangu ambaye tulipanga tuoane katika siku za mbele tutakapokuwa tayari. Sasa kitendo kile cha Saidi Omar kutaka kufunga uchumba na mimi kilikuwa ni kinyume na kile nilichokuwa nimepanga na mpenzi wangu.
Licha ya kwamba Alhakim alikuwa na uwezo, alikuwa mtu mzima sana na alikuwa na watoto wakubwa. Kwa vyovyote vile nisingeweza kuishi naye kwa amani. Yatakuwa ni mapambano kati yangu na watoto wake.
Lakini kwa vile wazazi wangu wametaka, nikanyamaza kimya huku nikiendelea kufikiria. Kuna siku nyingine nilikutana tena na Alhakim. Tulikutana Kariakoo. Mimi nilikuwa ninapita na hamsini zangu, yeye alikuwa akitoka katika duka la spea za magari.
Akaniona na kusimama.
“Habari yako?” Akaniuliza.
“Nzuri. Shikamoo…”
“Marahaba. Habari ya nyumbani?”
“Nzuri.”
“Baba anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri…”
“Mpaka pale mzee anaweza kutembea mwenyewe tunashukuru Mungu. Mimi nilihisi angekatwa mguu. Lakini tunashukuru sana,”
Alhakim akaniambia. Sikusema kitu. Nilikuwa nikitazama pembeni.
“Umepata salamu zangu?”
Akaniuliza.
“Kutoka wapi?”
“Kutoka kwa wazazi wako?”
Nikafahamu salamu zenyewe ni yale maneno niliyoambiwa na mama. Kwa vile nilikuwa ninamheshimu Alhakim, nilimwambia.
“Nimepata.”
“Umeridhika?”
“Bado ninafikiria.”
“Unafikiri nini Esma? Mimi nitakusubiri umalize masomo yako na ikiwezekana masomo yako nitayagharamia mimi hadi chuo kikuu. Ukimaliza masomo nitakununulia gari la kutembelea. Utaniambia unapenda gari la aina gani?”
Nilikuwa nimenyamaza nikiyafikiria maneno yake. Nilimtazama machoni kwa sekunde kama mbili tu kasha nikaugeuza uso wangu upande mwingine. Niligundua Alhakim alikuwa mtu mwerevu na mwenye hila.
Muda wote alikuwa akitabasamu. Kutokana na kile alichoonesha kuwa na uzoevu wa kuzungumza na wanawake, alikuwa habandui macho yake usoni kwangu. Yale macho yalikuwa na kazi ya kuzuga akili yangu ili maneno yake yaniingie.
“Kwani baba amekwambia nini?” Nikamuuliza.
“Baba yako nimeshakubaliana naye, umebaki wewe tu.”
“Kama mmeshakubaliana na baba, mimi nitasema nini?”
“Si umeniambia mpaka ufikirie?”
“Ni sawa. Binadamu unapoambiwa kitu lazima ufikiri. Huwezi kukubali tu. Kwa vile suala liko kwa wazazi watalimaliza wao.”
Mfu Aliyerudiwa na Uhai “Mimi nataka uniambie kwa kauli yako mwenyewe kwamba umeafikiana na uchumba wangu?”
Nikafikiri kidogo na kuona ni vizuri nimkubalie hivyo anavyotaka ili tusipoteze muda mrefu kwa suala hilo.
“Unachotaka wewe nikwambie tu kuwa nimeafikiana na uchumba wako?”
“Ndiyo.”
“Nimeafikiana nao…”
Mzee Alhakim akacheka kabla ya kuniambia. “Niambie kesho nitakuona wapi twende madukani nikufanyie shopping?”
“Nitakuwa nyumbani.”
“Si vizuri mimi kukufuata nyumbani kwa sababu pale kuna wazazi wako. Haitakuwa heshima kukufuata pale. Niambie mahali pengine.”
“Labda uniambie wewe.”
Alhakim aliwaza kidogo kasha akaniambia.
“Unakumbuka pale nilipokushusha na gari siku ile?”
“Ndiyo, ninapakumbuka.”
“Nisubiri pale.”
“Saa ngapi?”
“Saa nne asubuhi.”
“Si unafahamu kuwa saa nne nitakuwa shule labda nitakapotoka.”
“Unatoka shule saa ngapi?”
“Ninatoka saa tisa, lakini nitakusubiri pale saa kumi.”
“Hakuna tatizo kwa sababu saa kumi bado maduka yapo wazi. Nitakupitia saa kumi.”
Wakati tunataka kuagana alitia mkono mfukoni akatoa bunda la noti, akahesabu shilingi elfu hamsini akanipa.
“Chukua hii itakusaidia kwa usafiri.”
“Asante,” nikamwambia na kuzitia kwenye pochi yangu ndogo niliyokuwa nimeishika mkononi.
INAENDELEA, FUATILIA KISA HIKI MWANZO MPAKA MWISHO USIKOSE SEHEM YA KWANZA TUNAISHIA HAPA.
No comments
Post a Comment