Followers

Mwandila, Nsajigwa amrithi Lwandamina Yanga

Kanuni za Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Yanga inakaribia kuingia hatua ya makundi zikielekeza kwamba Kocha Mkuu ni lazima awe na leseni A inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaelekeza kwamba Kocha Mkuu wa timu inayoshiriki ligi hiyo anatakiwa anagalau awe na leseni daraja B ya CAF.

Dar es Salaam. Baada ya kocha George Lwandamina kutimkia Zesco United ya Zambia hivi karibuni, uongozi wa Yanga umemtangaza Noel Mwandila kuwa kocha mkuu hadi mwisho wa msimu mbali ya huyo wengine wenye uwezo wa kulibeba jukumu hilo ni Etienne Ndayiragije, Hans Pluijm, Juma Mwambusi, Masoud Djuma na Ally Bizimungu.

Ingawa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakimpigia chapuo kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa kupewa jukumu la kusimamia benchi la ufundi la Yanga moja kwa moja, viatu vya Lwandamina pamoja na matakwa ya kikanuni yanamzuia Nsajigwa kuwa kocha Mkuu wa Yanga kwa sasa.

Wakati kanuni za Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Yanga inakaribia kuingia hatua ya makundi zikielekeza kwamba Kocha Mkuu ni lazima awe na leseni A inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaelekeza kwamba Kocha Mkuu wa timu inayoshiriki ligi hiyo anatakiwa anagalau awe na leseni daraja B ya CAF.

"Kwa msimu wa 2017/2018 Kocha Mkuu wa timu ya kwanza ya klabu ya Ligi Kuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja B ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya Mabara mengine. Kuanzia msimu wa 2018/2019 na kuendelea Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja A ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya Mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA," kinafafanua kifungu cha 3 cha kanuni ya 71 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nsajigwa ana leseni daraja C ambayo kikanuni haimpi nafasi ya kuwa Kocha Mkuu wa Yanga kwa sasa ingawa pia bado anaonekana hajapata uzoefu wa kutosha kuhimili vishindo na presha zinazoikabili timu hiyo kwa kipindi hiki.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema hawana mpango wa kutafuta kocha mpya kwa sasa hadi mwishoni mwa msimu.

"Nsajigwa ni kocha msaidizi na itabaki kuwa hivyo wala vigezo vyake havimzuii kukaa benchi kama msaidizi, majukumu ya kocha mkuu kwa sasa yatakuwa chini ya Noel (Mwandila)," alisema Mkwasa.

"Mechi zilizosalia ni chache, hatuoni sababu ya kuleta kocha mpya, tutaajili kocha mwanzoni mwa msimu ujao," alisema Mkwasa.

Kocha wa kwanza anayeweza kunaswa kirahisi na Yanga ni Ndayiragije ambaye siku zake Mbao FC zimeanza kuhesabika kutokana na mfululizo wa matokea yasiyoridhisha ya timu hiyo yaliyochangia mashabiki kutaka kocha huyo ajiuzulu.

Kama hiyo haitoshi, Ndayiragije mwenye leseni daraja B inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya, hakuonekana kwenye benchi la ufundi la Mbao FC wakati ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Njombe Mji, Jumatano.

Katika kukoleza fununu za kocha huyo kutua Yanga, Mbao FC kwa sasa imemuongeza Fulgence Novatus ambaye ndiye amekuwa akisimamia mazoezi ya timu hiyo pasipo uwepo wa Ndayiragije ambaye hadi hajaweka bayana sababu za kutohuduria mazoezi hayo.

Akizungumzia taarifa za Yanga kutaka kumchukua Kocha wa Mbao, Mkwasa alisema kwa kifupi kuwa huo ni uvumi.

"Tuna mpango wa kuajili kocha, lakini siyo sasa na kuhusu kocha wa Mbao kuja Yanga huo ni uvumi tu," alisema Mkwasa.

Yanga ina uwezekano pia wa kumpata kocha wake msaidizi wa zamani, Juma Mwambusi ambaye kwa sasa hana timu anayoifundisha baada ya kuachana naye mwishoni mwa msimu uliopita.

Mwambusi ana leseni A ya ukocha kutoka CAF, anaifahamu vyema Yanga aliitumikia takribani miaka miwili akiwa msaidizi wa Hans Pluijm na baadaye Lwandamina hivyo ana uwezo mkubwa wa mashindano ya ndani na ya nje ingawa pia anabebwa na heshima aliyojijengea kwa wachezaji wa Yanga.

Kocha mwingine anayeweza kuirudisha Yanga katika mstari ni Pluijm wa Singida United kutokana na kocha huyo kuifahamu vyema klabu hiyo baada ya kuinoa kwa nyakati mbili tofauti na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili, kutwaa ubingwa wa Kombe la FA msimu wa 2015/2016 pamoja na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016.

Hata hivyo, Yanga ina kibarua kigumu kumnasa Pluijm ambaye pia ni mwanachama wake kwani italazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumshawishi avunje mkataba wake na Singida United, pia kuna tetezi kuwa ameshafikia makubaliano ya kuwa kocha mkuu wa Azam FC  msimu ujao.

Kuhusu kuhusishwa kwake na Yanga, Kocha Pluijm aliliambia gazeti hili kwa sasa anaheshimu mkataba wake na Singida United.

"Siyo Yanga tu bali pia nimekuwa nikihusishwa kujiunga na Azam FC, lakini kwa upande wangu niseme wazi kwamba nina mkataba na Singida United na akili na malengo yangu kwa sasa ni kuisaidia timu yangu ifanye vizuri katika mashindano yaliyo mbele yetu na sio kushughulika na hizo habari zinazozushwa huko pembeni," alisema Pluijm.

Kocha mwingine anayeweza kutua Yanga kwa kipindi hiki ni Ally Bizimungu wa Mwadui FC ameweza kuibadili timu hiyo na kuiondoa kwenye janga la kushuka daraja tofauti na alivyoikuta.

Kocha huyo aliikuta Mwadui ikiwa na pointi tisa tu kwenye msimamo wa ligi katika mechi 11 ilizokuwa imecheza ikipata ushindi mara moja na kutoka sare sita huku ikipoteza mechi nne lakini baada ya ujio wake, Mwadui imecheza michezo 13, ikishinda mechi nne, kutoka sare mitano na kupoteza minne.

Bizimungu alisema yuko tayari kujiunga na Yanga ikiwa watamhitaji ingawa ni lazima aagane vizuri na Mwadui.

"Binafsi nimekuja Tanzania kufanya kazi hivyo kama nafasi ya kufundisha timu kama Yanga inakuja, ni vigumu kuiacha ipite ingawa hilo litafanyika baada ya kupata baraka za Mwadui ambao ndio wamenileta hapa Tanzania.

“Nimesomea ukocha Ujerumani kwa lengo la kuwa kiongozi wa benchi la ufundi na siyo kuwa msaidizi hivyo sharti langu kuu kwa timu yoyote itakayonihitaji ni kwamba nataka niwe kocha mkuu," alisema Bizimungu.

Yanga pia inaweza kujaribu bahati yake kwa kocha msaidizi wa Simba, Masudi Djuma aliyeonyesha uwezo wa hali ya juu wa kusimamia timu kutokana na mbinu zake nyingi za kiufundi, lakini anakosa nafasi ya kutosha kuthibitisha ufanisi wake kutokana na kulazimika kutekeleza kile anachopangiwa na Kocha Mkuu wake Pierre Lechantre.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.