Sakata la Makonda latua bungeni
Sakata la Makonda latua bungeni
SUALA la mamia ya wanawake kufurika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulalamika kwamba wametelekezwa na watoto wao, limepiga hodi bungeni.
Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) ameibua hoja hiyo huku akishangiliwa na wabunge, wakati alipoomba mwongozo wa Spika, akiomba serikali itoe ufafanuzi kuhusu jambo linaloendelea Dare es Salaam la kutafuta wanaume waliotelekeza watoto. Mlinga alisema kinadharia jambo hilo ni jema, lakini kiukweli njia inayotumika, inabomoa badala ya kujenga jamii na familia nyingi nchini.
Akinukuu Ibara ya 16 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mlinga alisema kifungu hicho kipo kwa ajili ya kulinda faragha na maisha ya mtu. Ibara hiyo inasema, “Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi”.
Lakini, Mlinga alisema kitendo kinachofanyika Dar es Salaam ni cha kutoa uwanjani mambo yaliyofanyika sirini. Alisema hata Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inamlinda mtoto na kueleza kwamba hatakiwi kuoneshwa hadharani au kwenye vyombo vya habari. Hivyo, alisema kitendo cha kuwaonesha watoto na kudai wanafanana na mtu fulani, kinajenga uadui wa kudumu.
Pia katika hali ya kawaida, Mlinga alisema suala hilo badala ya kutafuta suluhu, linalenga kugombanisha baba na mama katika familia moja, kwani hata kwa mujibu wa dini ya Kiislamu mtoto anayezaliwa nje ya ndoa ni haramu, hivyo kuweka hadharani ni kuharibu ndoa za watu. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema hana cha kusema kutokana na mtu aliyesema alitelekeza mtoto. Lakini aliongeza kwamba mambo hayo yanayofanyika hayana ukweli wowote. Alieleza kuwa kama anasemwa kwamba alitelekeza mtoto, basi afikishwe bungeni na ikibainika ni kweli, yupo tayari kuachia ubunge.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga alisema masuala hayo ni ya kisheria, lakini hakuna uthibitisho wowote kuhusu mbunge au watoto. Giga alisema maadamu ni mchakato unaoendelea, ukimalizika itajulikana, lakini kama kuna mtu atabainika kuwa ametelekeza, kila mtu atabeba wajibu wake kisheria.
Katika tukio jingine, vilio vya furaha na vigelegele vilitawala jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, baada ya kutangazwa utolewaji bure wa huduma ya afya kwa watoto wote waliotelekezwa na baba zao na kupelekwa na mama zao kwenye ofisi hiyo kulalamikia matunzo. Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Makonda alitangaza watoto hao kukatiwa kadi za bima ya afya, alipozungumza na wanawake hao asubuhi jana. Makonda alisema wakati ofisi yake ikiendelea na harakati za kuwasaidia wanawake waliotelekezwa, kuna tajiri mmoja ambaye ameguswa na harakati hizo na kuamua kumuunga mkono, kwa kuwasaidia watoto wanaoteseka, kwa kukosa huduma ya uhakika ya afya.
No comments
Post a Comment