Followers

Vumbi la April 26


Dar/ mikoani. Wakati Marekani na Uingereza zikitoa tahadhari kwa raia wake waliopo hapa nchini kuhusu maandamano yanayopangwa mitandaoni kufanyika kesho, polisi wamewakamata watu wanaodaiwa kuyaratibu.

Sambamba na hilo, katika baadhi ya mikoa polisi wamefanya mazoezi ya utayari.

Februari mwaka huu, kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwataka Watanzania kujiepusha na maandamano yanayoratibiwa mitandaoni akionya atakayeshiriki atakuwa amevunja sheria.

Aprili 26 ni siku ya mapumziko ambayo Watanzania wataadhimisha miaka ya 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Maadhimisho kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.

Serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake nchini imetoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi Tanzania kuhusu maandamano hayo ukisema wanapaswa kuwa makini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, ubalozi huo umesema polisi wamejiandaa kukabiliana na maandamano hayo.

“Polisi huenda wakatumia mabomu ya machozi na risasi za moto ili kudhibiti maandamano hayo, hivyo ni muhimu kukaa mbali na waandamanaji hao,” imesema taarifa hiyo.

Serikali ya Uingereza kupitia ubalozi wake hapa nchini pia imewataka raia wake kuchukua tahadhari.

Taarifa ya ubalozi huo kwa vyombo vya habari jana ilisema kuna raia zaidi ya 75,000 wa Uingereza wanaoingia Tanzania kila mwaka.

Ubalozi umewataka kutojihusisha na maandamano kwa maelezo kuwa wanaweza kupata madhara kutoka kwa polisi ambao wamedhamiria kupambana na waandamanaji.

“Muwe makini mnapokuwa kwenye mizunguko yenu, muepuke mikusanyiko ya watu au watu wanaoandamana, muda wote msikilize vyombo vya habari mjue nini kinachoendelea. Ikiwa mnahitaji mawasiliano namba ya dharura ya kupiga ni 112 uliza huduma ya dharura unayohitaji,” inasema taarifa hiyo.

Pia, raia hao wa Uingereza wanashauriwa kuwa makini wawapo barabarani na wawasiliane na ofisi za ubalozi wanapohitaji msaada wowote.

Mkoani Arusha, watu saba wamekamatwa na polisi wakituhumiwa kuhamasisha maandamano kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Yusuph Ilembo alisema kukamatwa kwao kunatokana na upelelezi unaoendelea.

Alisema kwa takriban mwezi mmoja kuna watu wanahamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Telegram.

Kamanda Ilembo alisema upelelezi unaofanywa na kikosi maalumu cha intelijensia umewezesha kukamatwa kwa watu hao wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu.

“Napenda kutumia fursa hii kuwataka wakazi wa Arusha kuachana na maandamano kwani Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi,” alisema.

Ilembo alisema wanafunzi na wanavyuo wanapaswa kusoma kwa kuwa wazazi wao wanajua kuwa wako masomoni, lakini baadhi wanafanya vitendo vinavyovunja sheria.

Hata hivyo, kamanda huyo hakuwataja majina watuhumiwa akisema upelelezi unaendelea.

Machi 21, polisi mkoani Dodoma iliwakamata watu wawili kwa kosa la kuhamasisha maandamano mtandaoni huku juzi wengine watatu wakikamatwa.

Polisi mjini Morogoro jana walifanya doria katika mitaa ya manispaa hiyo wakiwa na mbwa, magari ya maji ya kuwasha na askari wenye silaha za moto na mabomu ya machozi.

Baada ya doria iliyoanza saa tatu asubuhi hadi saa tano, kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema ni ya kawaida yenye lengo la kupambana na matukio ya uhalifu.

Alisema ni kawaida kwa jeshi hilo kufanya doria ili kujiweka tayari kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kutokea kwa kupangwa. “Jeshi la Polisi halitamuonea haya mtu au kikundi cha watu chenye lengo la kuvunja amani au kufanya uhalifu wa aina yoyote,” alisema.

Mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wakazi wa Mji wa Moshi waliingiwa na taharuki baada ya polisi kufanya mazoezi ya kukimbia barabarani wakiwa wamebeba silaha.

Askari hao wengi wakiwa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walikuwa wamevaa mavazi maalumu ya kujihami na ghasia.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Khamis Issah alisema ni mazoezi ya kawaida kwa askari hao.

“Askari wetu walikuwa wakipata mafunzo ya nadharia kwa muda mrefu, kwa hiyo tumeamua kufanya kwa vitendo,” alisema Kamanda Issah.

Baadhi ya maeneo waliyopita askari hao ni Majengo, Pasua, Shanti Town na Soweto.

Polisi Zanzibar imewaonya Wazanzibari wenye dhamira ya kujihusisha na ‘maandamano’ ya Aprili 26.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Haji Hassan alisema wana taarifa zilizosambaa mitandaoni za kuhamasisha maandamano hayo, hivyo hawatakuwa tayari kuona amani inachafuliwa.

Alisema wataimarisha ulinzi siku hiyo ambayo wananchi wataadhimisha miaka 54 ya Muungano na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa kina kuwabaini wanaojihusisha na uhamasishaji wa maandamano hayo kupitia mitandao.

Imeandikwa na Janeth Joseph (Moshi), Muhammed Khamis (Zanzibar), Hamida Shariff (Morogoro) na Mussa Juma (Arusha)

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.