Followers

Wanaobeza Serikali Kukopa Fedha Mtafakali Kwanza :Dkt John Magufuli



Rais John Magufuli amesema Serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hata kama kuna watu wanabeza.

Amesema fedha hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu na kwamba fedha hizo ndizo hutumika kujenga miundombinu kama barabara ili kuchochea uchumi.

Rais alisema hayo jana mjini Iringa alipofungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa kilomita 189 inayounganisha mikoa ya Iringa na Dodoma. Tukio hilo lilirushwa hewani moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC 1.

Barabara hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh207.4 bilioni ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri.

Imejengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jica) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania asilimia 12.8.

“Msiwasikilize wanaosema Serikali ina madeni makubwa wakati wao wenyewe wanapita kwenda bungeni kwenye barabarani tulizozijenga kwa kukopa,” alisema.

Magufuli alisema Serikali imekuwa ikidaiwa tangu enzi za mkoloni, lakini madeni mengine yamekuja kulipwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumzia barabara hiyo, Rais alisema inalenga la kuimarisha utalii katika ukanda wa kusini.

“Watu walizoea (kwamba) ukitaka kutalii ni lazima uende Serengeti wakati Ruaha ni mbuga kubwa yenye vivutio bora, lakini haikutembelewa na watalii kwa sababu ya ukosefu wa barabara,” alisema.

“Kwa sasa itabidi wenzetu wa kaskazini wasubiri kwanza. Kwa sasa tunaendeleza maeneo yaliyochelewa kuendelezwa,” alisema.

Rais Magufuli alisema Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo Iringa utaimarishwa ili watalii waweze kufika maeneo ya utalii.

Rais Magufuli alisema barabara hiyo pia itawasaidia wakazi wa Iringa kusafirisha mazao kwenda sokoni bila matatizo.

“Barabara hii iwe mkombozi wa maisha yetu. Tuitunze, itasafirisha mazao, mtasafiri kwa utulivu kwenda kwenye shughuli zenu,” alisema.

Magufuli ambaye alisoma Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa kuanzia mwaka 1978/79, alisema anakumbuka hali ya barabara ilivyokuwa tatizo wakati huo.

“Kutoka Dodoma hadi Iringa nilitumia siku mbili kwa kutumia basi la Shirika la Reli Tanzania. Tulilala njiani kwa sababu ya ubovu wa barabara,” alisema.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.