Wasioendeleza ardhi Kigamboni kuporwa
Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa ametoa siku 30 kuendeleza maeneo wanayoyamiliki katika wilaya hiyo vinginevyo watanyang’anywa na kupewa wawekezaji wenye kuyahitaji.
Akizungumza jana, Mgandilwa amesema hayo leo Aprili 9 kwamba lengo si kuwanyang’anya watu ardhi wanayoimiliki bali ni kutaka ardhi iendelezwe.
Alisema uongozi wa wilaya hiyo ulitembelea maeneo mbalimbali na kubaini kwamba asilimia 70 ya fukwe zake hazijaendelezwa.
“Baadhi ya fukwe ni vichaka ambavyo vimegeuka kuwa maficho ya vibaka, hatuwezi kuacha hali hii iendelee,” amesema
Amesema wenye maeneo hayo wanatakiwa kuyaendeleza kabla hayajanyang’anywa kwa kuwa kuna watu wanahitaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli na viwanda.
Amesema ili wananchi waweze kuendeleza maeneo yao, amewaagiza watendaji kutoa vibali vya ujenzi ndani ya siku tano badala ya siku 30.
“Lengo ni kuwahamasisha watu kuendeleza maeneo yao badala ya kuyaacha yaendelee kuwa mapori,” amesema .
Mgandilwa amesema Rais John Magufuli aliivunja Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) na kwamba shughuli zote sasa zinafanywa na halmashauri ya wilaya ya Kigamboni.
“Mamlaka hiyo haikuruhusu watu kuendeleza maeneo yao lakini sasa ruksa kuendeleza kwa kufuata sheria zilizopo,” amesema.
Kuhusu ujenzi ufukweni, mkuu wa wilaya alisema wako watu wanaojenga ufukweni na kuingia ndani ya mita 60 kinyume na sheria.
“Ujenzi katika maeneo hayo unahitaji vibali maalum kwa majengo yasiyo ya kudumu,” amesema.
Mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji wa wilaya hiyo, Dotto Msawa aliwakaribisha wafanyabiashara kuwekeza katika eneo la Kigamboni kwa kuwa bado kuna ardhi kubwa inayohitajika kwa ajili ya uwekezaji.
“Bado Kigamboni ina ardhi inayofaa kwa ajili ya viwanda, hoteli na maghala, hapa ni kilometa chache kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam lakini unaweza kupata ardhi yenye ukubwa unaohitaji,” amesema .
Ofisa mipango miji wa halmashauri ya wilaya ya Kigamboni, Nice Mwakalinga alisema watahakikisha vibali vinatolewa ndani ya siku tano.
“Tulikuwa tunatoa vibali ndani ya siku 30 lakini sasa tumejipanga kivitoa kwa siku tano, tunawakaribisha,” amesema
No comments
Post a Comment