Followers

Waziri Mwakyembe Awaasa Watanzania Kupambana Na Viashiria Vinavyo Sababisha Mauaji Ya Kimbari



Na: Mwandishi wetu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe, amewaasa Watanzania kuhakikisha wanapambana na viashiria vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na mauaji ya kimbari. Kauli hiyo  Dkt. Mwakyembe ameitoa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu za mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka 24 iliyopita.

Kwenye hotuba yake Dkt. Mwakyembe amesema mauaji ya kimbari hayatokei ghafla bali huanza kwa chokochoko na kauli za kichochezi ambazo zina lengo la kuigawa jamii vipande vipande. 

“Kilichotokea Rwanda ni fundisho kwetu, mauaji ya kimbari hayatakiwi kutokea tena. Kuhakikisha hayatokei lazima tuyadhibiti mambo yote yanayoweza kuligawa taifa kwa faida ya kizazi cha leo, kesho na keshokutwa” Dkt. Mwakyembe alisisitiza.

Kuendelea kutia mkazo wa ujumbe wake Dkt. Mwakyembe aliinukuu kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, aliyoitoa wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda  ambapo alisema “haya hayatatokea tena, hatuwezi kubadili kilichotokea awali, lakini tunaweza kubadilisha hali ya leo na hata ya baadae”.

Balozi wa Rwanda nchini mheshimiwa Eugine Kayihura ameishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwa pamoja na Wanyarwanda. Pia ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kindugu kati ya Tanzania na Rwanda kwa maendeleo ya watu wake.

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez amesema nchi zote zina wajibu wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Pia zinatakiwa kuhakikisha zinaungana kupambana na mtu au kikundi chochote chenye nia ya kutekeleza uhalifu kama huo.

Kumbukumbu za mauaji ya kimbari ya Rwanda huadhimishwa kila mwaka na mwaka huu maadhimisho hayo kwa Tanzania yamefanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ambapo Dkt. Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, watu mashuhuri, viongozi wa serikali na mashirika ya kimataifa na wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dar-es-salaam

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.