CCM, Chadema ‘zavuruga’ uchaguzi wa Daruso
Uchaguzi wa viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) umegubikwa na siasa za chama tawala na upinzani.
Kutokana na siasa hizo, inaelezwa kuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi chuoni hapo, Kambarage Kinemo na katibu wake, Ishengoma Ladislaus walikamatwa juzi wakiwa ofisi ya mshauri wa wanafunzi chuoni hapo na kufikishwa kituo cha polisi Kijitonyama wakituhumiwa kwa wizi wa simu ya mkononi.
Chanzo cha habari kimeieleza Mwananchi kuwa wawili hao walikamatwa saa chache baada ya urejeshaji fomu za wagombea urais na makamu wa rais wa Daruso kukamilika.
Inaelezwa kuwa tuhuma dhidi yao zilitengenezwa na uongozi wa Daruso ulio madarakani baada ya kukaidi kupitisha majina ya wagombea walio katika mrengo wa kisiasa wanaoutaka wao.
“Hapa chuoni hawapendi Daruso iongozwe na wanafunzi kutoka .... sasa ile tume ni watu ambao hawataki kusikiliza mtu, viongozi waliopo madarakani walitaka kupitishwa wagombea wao...wasimamizi walikataa,” kilisema chanzo hicho.
“Fomu zilikuwa zinarudishwa leo (jana) ili majina yahakikiwe na kupitishwa kugombea, kwa sababu kulikuwa na mgomo wa wasimamizi wa tume kupitisha majina ya wagombea wa chama (jina tunalo), ikabidi watengenezewe skendo ya wizi wa simu ya mkononi kabla ya kupitishwa majina hayo,” kilieleza chanzo hicho.
Kambarage na Ishengoma walichaguliwa kuongoza tume hiyo Aprili 25 na walishiriki kuendesha uchaguzi wa viongozi wakiwamo wa vitivo uliofanyika Mei 10.
Polisi Mkoa wa Kinondoni imekiri kuwa wasimamizi hao walihojiwa kwa saa kadhaa na kuachiwa kwa dhamana.
“Ni kweli walikamatwa na kuhojiwa lakini waliachiwa jana (juzi) hiyohiyo, sasa mtuhumiwa hatumwangalii cheo, rangi, kabila, wewe ukifanya kitu cha kijinai watu wakija kushtaki hatuwezi kusema tunayemkamata au tunayemuhoji ni mwandishi wa habari, japokuwa watu watasema mbona mwandishi wa habari?” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro.
Alisema wamewahoji na wametoa maelezo na upelelezi unaendelea na kwamba, suala hilo linaweza kuonekana dogo kwa watu wengine, lakini linaweza kuwa kubwa kwa mtu aliyeathiriwa.
Rais wa Daruso, Jeremiah Jilili aliliambia Mwananchi kuwa walikamatwa wakiwa wameshamaliza jukumu lao la kupitisha majina ya wagombea mchana.
Jilili alisema hawezi kuzungumzia tuhuma za wizi wa simu kwa kuwa hakuwapo. Pia alikana tuhuma za kuandaa viongozi wanaotokana na vyama vya siasa.
“Daruso tuna utaratibu mzuri wa kuandaa viongozi kwa hiyo suala la viongozi binafsi kuandaa sidhani kama linawezekana, hayo mazingira sijayaona, kuna tume huru inayochaguliwa, ukifanya connection ya kilichotokea na uchaguzi huu hakuna uhalisia… lakini kama tunazungumzia wizi halafu mtu kaiba halafu akikamatwa unasema ni kwa sababu ya uchaguzi, hiyo ni coincidence inatokea,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi alisema umoja wa vijana wa vyuo vikuu chini ya baraza hilo (Chaso) haujihusishi na siasa na kwamba hawana taarifa ya vijana wa Chaso kugombea.
Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James alisema kwa namna yoyote ile CCM haiwezi kujihusisha na uchaguzi wa Daruso. “Tuna wanachama ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini, hakuna ambapo CCM tunapeleka mgombea haipo katika utaratibu wetu.”
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi Mei 17, kampeni za uchaguzi nafasi ya rais na makamu wa rais zitaanza na uchaguzi utafanyika Juni Mosi.
Profesa Mohammed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema siasa ndani ya jumuiya za wanafunzi vyuoni ikiwamo UDSM imekuwapo kwa muda mrefu na imeshatengeneza makundi mawili ya vyama vikubwa vya CCM na Chadema.
Alisema tangu vyama hivyo vianze kuingia katika jumuiya hizo, serikali za wanafunzi zimekuwa zikikosa nguvu ya kujadili maslahi yao kwa pamoja.
Ni mara chache kuona sasa hivi wanakaa pamoja kujadili amsuala yao, huwezi kuona wakikemea serikali kuhusu jambo linalokwenda kinyume na maslahi yao, ni kwa sababu tayari vyama hivyo vimeshawagawa,”alisema Profesa Bakari.
Profesa Bakari alisema kabla ya miaka ya 1990, serikali za wanafunzi vyuoni zilikuwa na nguvu ya kukosoa au kupongeza jambo lolote kwa kauli moja katika jamii au serikali bila kuwa na mpasuko ,lakini hali hiyo haipo tena.
Wakati huohuo, akizungumzia na waandishi wa habari jana, katibu wa itikadi, mawasiliano na uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema wanapinga kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa akiwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) wiki iliyopita ya kuzuia siasa vyuoni.
Shaibu alisema hilo linahatarisha uthubutu wa vijana na itazalisha walio waoga.
Shaibu alisema historia inaonyesha viongozi wengi wa Taifa walishawahi kuwa viongozi wa serikali za wanafunzi walipokuwa vyuoni, akisisitiza maisha ya siasa wakiwa vyuoni ndiyo yaliwapa ujasiri wa kuingia kwenye ulingo wa siasa.
“Kupiga marufuku siasa vyuoni ni kujenga Taifa la vijana waoga, wasiokuwa na uwezo wa kuhoji. Vijana msiache kuhoji mambo ya msingi kwa jamii zenu, hiyo ndiyo maana ya kuitwa wasomi,” alisema Shaibu.
No comments
Post a Comment